Trump amchagua Seneta JD Vance kama mgombea mwenza
16 Julai 2024Haya yanafanyika chini ya siku mbili baada ya Trump kuponea chupuchupu jaribio la kumuua katika mkutano wa kampeni huko Pennsylvania.
Tangazo hilo la kumchagua Trump kama mgombea wa urais pia limetolewa muda mfupi baada ya mgombea huyo kumtangaza seneta wa jimbo la Ohio JD Vance kama makamu wa rais na mgombea mwenza wake.
Trump amemchagua Vance kama mgombea mwenza wake wakati ambapo wajumbe wa chama hicho walikuwa bado wanapiga kura ya kumchagua atakayeipeperusha bendera yao katika uchaguzi.
Kura ya wajumbe wa Republican kwa Trump inahakikisha kwamba ni wazi sasa rais huyo wa zamani wa Marekani, atakiongoza chama hicho kwa mara ya tatu mfululizo kama mgombea wao katika uchaguzi mkuu.
Kutupiliwa mbali kwa kesi ya nyaraka za siri
Mwanawe Trump Eric, ndiye aliyetangaza matokeo ya kura hiyo ya wajumbe huko Florida huku televisheni zilizokuwa katika chumba hicho cha mkutano huo zikionesha maneno "juu zaidi" baada ya Trump kutangazwa mshindi. Wimbo wa sherehe ulipigwa huku wajumbe wakionekana wakicheza wimbo huo na kuonesha mabango ya Trump.
Baadhi ya wajumbe walisikika wakiimba "pambaneni, pambaneni"maneno yale yale aliyokuwa akiyasema Trump wakati alipokuwa akiondolewa jukwaani siku chache zilizopita baada ya kunusurika jaribio la kumuua wakati wa kampeni huko Pennsylvania.
Habari nyengine iliyopokelewa vyema na wajumbe wa Republican ni kwamba jaji aliyekuwa anaisikiliza kesi ya nyaraka za siri iliyokuwa inamkabili Trump ameitupilia mbali kesi hiyo na kumpa ushindi mkubwa wa kortini Trump.
Maandamano nje ya Mkutano Mkuu wa Republican
Mbali na kumchagua rasmi Trump kama mgombea wa chama hicho, wajumbe kutoka kote nchini Marekani watageukia katika kuweka sera mpya katika jukwaa la sera la chama hicho, jambo hilo likiwa linafanyika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2016.
Hatua hiyo inaonesha kwamba timu ya kampeni ya Trump haina nia ya kuwapa Wademocrat mada yoyote ile watakayoitumia katika kampeni yao, kwani waraka huo wa sera za chama cha Republican unazungumzia masuala muhimu likiwemo suala tata la uavyaji mimba.
Kwa sasa Wademocrat wamepunguza mipango yao ya kutoa ujumbe wa ushindani wakati wa mkutano huo mkuu wa chama cha Republican na wameyaondoa matangazo yao ya kampeni hasa kufuatia jaribio la kumuua Trump.
Nje ya mkutano huo mkuu wa chama cha Republican huko Milwaukee, mamia ya waandamanaji wamekusanyika wakisema jaribio la kumuua Trump halitoisitisha mipango yao ya muda mrefu ya kuandamana nje ya jengo linakofanyika mkutano huo.
Wanaharakati hao wanasema masuala kama haki ya uavyaji mimba, haki ya kiuchumi na vita vinavyoendelea Gaza ni mambo yanayostahili kupewa kipau mbele.
Chanzo: AP