Trump aitaka NATO kutumia 5% ya Pato la Taifa kwa ulinzi
10 Januari 2025Kauli ya Rais mteule wa Marekani Donald Trump ya kuwataka washirika wa NATO kutumia asilimia 5 ya pato jumla la taifa kwa mwaka katika ulinzi umeibua mijadala katika miji mikuu ya Ulaya siku kadhaa kabla ya Trump hajarejea katika Ikulu ya White House.
Hilo ni ongezeko kubwa ukilinganisha na ahadi ya asilimia 2 ambayo washirika wa NATO walikubaliana, lakini ambayo pia ilionekana kuwa ngumu kutekelezeka kwa mataifa kadhaa ya Ulaya. Lakini kiwango hicho ni kikubwa zaidi kuliko asilimia 4 aliyoitaka Trump alipokuwa rais.
Katika mkutano wa kilele wa NATO mjini Washington mwaka jana, muungano huo wa kijeshi ulifichua kwamba mwaka huu, angalau theluthi mbili ya wanachama wake walitumia asilimia 2 au zaidi katika ulinzi huku Poland ikiwa nchi pekee iliyozidi asilimia 4. Wachambuzi wanasema matakwa ya Trump yanaweza kuwa tu ni mbinu ya kujiandaa kufikia mwafaka katika mazungumzo yajayo.
Soma pia: Changamoto za NATO 2025: Trump, Ukraine na matumizi ya ulinzi
Hata hivyo, mataifa ya Ulaya yatalazimika kuwekeza zaidi ili kufufua bajeti za ulinzi na kukabiliana na uwezekano wa vitisho vya Urusi. Hata hivyo, wachambuzi kadhaa wameiambia DW kwamba kuongeza bajeti ya ulinzi hadi asilimia 5 inaonekana ni jambo lisilowezekana hata kwa mataifa tajiri hasa ukizingatia hali ya sasa ya kiuchumi.
Kutaja asilimia 5 ili kujiandaa kukubali asilimia 3.5?
Baadhi ya wachambuzi wanasema matakwa ya Trump ya asilimia 5 huenda ni mbinu tu ya kujiandaa ili kufikia mwafaka katika mazungumzo yajayo. Rafael Loss, mtaalamu katika Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni (ECFR) anasema ongezeko la asilimia 3.5 linaweza kutekelezeka kwa mataifa ya Ulaya na kwamba nchi wanachama bila chaka watafikia muafaka. Lakini akatahadharisha kuhusu hatua ya Trump kuiondoa Marekani kwenye NATO na hivyo kupelekea Putin kufanya anachotaka.
Ian Lesser, mkuu wa taasisi ya Ujerumani ya Marshall Fund nchini Ubelgiji anasema mahitaji ya hivi punde ya Trump yanaonekana kimsingi kama njia ya kufungua mjadala na bila shaka anaweza kuafiki hata kiwango kilicho chini ya hicho hasa ikizingatiwa kuwa kwa wanachama wengi wa Ulaya wanaweza kufikia asilimia 3 hadi 3.5.
Mkuu wa NATO: "Msiisahau Urusi"
Mwezi Desemba mwaka jana, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Mark Rutte aliiukumbusha umma wa Ulaya kuwa bajeti ya ulinzi ya Urusi inakadiriwa kufikia asilimia 7 hadi 8 ya Pato jumla la Taifa na kusema kuwa Ulaya inahitaji kujiandaa na vita na kuimarisha ulinzi wa bara hilo.
Alitoa wito kwa nchi wanachama kupunguza sehemu ya bajeti zao zinazotumika kwa ajili ya ustawi wa jamii na kuzitumia zaidi katika ulinzi.
Soma pia: Katibu Mkuu wa NATO kumshawishi Trump juu ya mkataba wa silaha
Rutte aliskika akisema kuwa kwa wastani, nchi za Ulaya hutumia hadi robo ya mapato yao ya kitaifa kwa ajili ya pensheni, afya na mifumo ya hifadhi ya jamii, na kwamba kinachohitajika ni kutumia sehemu ndogo ya pesa hizo ili kuufanya ulinzi wa Ulaya kuwa na nguvu zaidi, ili kuendelea kutetea mfumo wetu wa maisha.
Hadi sasa, hakuna mwanachama wa NATO anayetumia asilimia 5 ya Pato jumla la Taifa kwa ulinzi, hii ikiwa ni kulingana na takwimu za muungano huo wa kijeshi. Poland ndiyo inayotumia pesa nyingi zaidi kwa asilimia 4.12 ya Pato la Taifa, ikifuatiwa na Estonia (3.43%), Marekani (3.38%). Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz ameeleza upinzani wake dhidi ya mwito huo wa Trump akisema kiwango hicho ni kikubwa mno.
(DW)