NATO kuzungumza na Trump kuhusu mkataba wa silaha
9 Januari 2025Mark Rutte anajaribu kukabiliana na msukumo wa Trump wa kutaka mabadiliko na hofu kwamba ataendeleza shinikizo zaidi kwa washirika wa Ulaya kuwekeza zaidi kwenye ulinzi.
Siku ya Jumanne, Trump alitoa wito kwa nchi za NATO kuongeza bajeti zao za ulinzi kutoka asilimia 2 hadi 5 ya pato lao la taifa baada ya kusema mara kwa mara kuwa wanachama wa muungano huo hawakufanya vya kutosha kuhakikisha ulinzi wao.
Kwa muda mrefu Trump amekuwa akiwakosoa wanachama wa NATO kwa kuwekeza kidogo katika ulinzi huku wakitegemea pakubwa ulinzi wa Marekani. Wakati wa muhula wake wa kwanza, Trump alitishia kuiondoa Marekani katika muungano huo wa kijeshi wa NATO kutokana na suala hilo.
Rutte anatarajiwa baadaye leo kutoa maoni yake kuhusu kauli hiyo ya Trump, lakini akasema kuwa Ulaya inahitaji mifumo ya ulinzi wa anga chapa Patriot na kwamba mengi yangeliweza kufanyika ikiwa sekta ya ulinzi ya Marekani ingekuwa huru na kuondoa haja ya kupata idhini kutoka kwa baraza la Congress, Wizara ya Ulinzi ya Pentagon na hata Ikulu ya White House.
Soma pia: Changamoto za NATO 2025: Trump, Ukraine na matumizi ya ulinzi
Katibu Mkuu huyo wa NATO, amesema Marekani itapata faida kubwa kwa kuiuzia Ulaya mifumo hiyo ambapo mfumo mmoja wa Patriot unagharimu dola bilioni 2, jambo ambalo ni bora kwa uchumi wa Marekani. Hata hivyo, amesema inachukua muda mrefu sana kuiwasilisha mifumo ya Patriot hadi barani Ulaya
Kanuni mpya kupunguza mivutano ya kisiasa
Udhibiti utaweza kuzuia migogoro na kuyawezesha mataifa ya Ulaya kuwekeza zaidi kwenye ulinzi, lakini pia utamuwezesha Trump kunadi mafanikio ya uimarishwaji wa sekta ya ulinzi ya Marekani.
Kulegezwa vizuizi vya ununuzi wa silaha za Marekani kunaweza pia kupunguza mivutano ya kisiasa itokanayo na ununuzi wa silaha kutoka nchi zisizo wanachama wa NATO. Kwa mfano, hatua ya Uturuki kununua mfumo wa ulinzi wa anga wa S-400 kutoka Urusi ilizua mivutano kwa miaka kadhaa. Uturuki ilijitetea kwa hoja kuwa ilishindwa kwa muda mrefu kupata mfumo wa Ulinzi wa Marekani wa Patriot.
Soma pia: Kauli za Trump zakemewa vikali na viongozi duniani
Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte amekuwa akisisitiza mara kwa mara haja ya mataifa ya Ulaya kuongeza bajeti zao za ulinzi, huku akitahadharisha kuwa katika kipindi cha miaka minne hadi mitano ijayo, itakuwa vigumu kukabiliana na Urusi ikiwa bajeti hizo za ulinzi hazitaongezwa.
Wachambuzi wanahisi kuwa huenda NATO ikapitia kipindi kigumu zaidi katika historia yake chini ya muhula huu wa Trump anayetarajiwa kuapishwa Januari 20, 2025.
(Chanzo: DPA)