TPLF waudhibiti tena mji wa Lalibela
13 Desemba 2021Haya ni kwa mujibu wa wakaazi wa eneo hilo waliozungumza na shirika la habari la AFP, siku 11 baada ya vikosi vya Ethiopia kusema kwamba vimedhibiti tena eneo hilo.
Tangazo hilo linaashiria mabadiliko mengine makubwa katika mzozo uliodumu kwa miezi 13 ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuibua mzozo mkubwa wa kibinadamu kaskazini mwa taifa la pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika.
Kulingana na baadhi ya wakaazi wa eneo hilo wapiganaji wa Tigray wamerudi katikati mwa mji wa Lalibela, wakionekana kutokea upande wa mashariki mwa mji wa Woldiya. Taarifa zinaashiria kuwa watu wengi wanakhofu, wengine wanakimbia makaazi yao na kwamba wengine wengi, tayari wameondoka kwa kuhofia mashambulizi ya kulipiza kisasi, baada ya kudhihirisha furaha yao wakati jeshi lilipoondoka.
soma Jeshi limeukomboa mji wa Shewa Robit, Ethiopia
TPLF imeanzisha mashambulizi makubwa
Uongozi wa kijeshi wa kundi la wapiganaji wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray, (JWTZ) ulisema katika taarifa iliyosambazwa na vyombo vya habari vinavyowaunga mkono kuwa wameanzisha mashambulizi makubwa katika maeneo mengi ikiwa ni pamoja na barabara inayounganisha Gashena na Lalibela. soma Ni marufuku kutoa taarifa za harakati za kijeshi Ethiopia
Jumapili jioni,kundi hilo lilisema kuwa baada ya kuangamiza na kutawanya jeshi kubwa la adui lililowekwa ndani na karibu na mji wa Gashena wameuteka tena mji huo na eneo linalouzunguka na pamoja na uwanja wa ndege wa Lalibela na mji wa Lalibela.
Hata hivyo serikali haikujibu maombi ya shirika la habari la AFP kuhusu taarifa hizo. Mawasiliano yamekatika katika eneo la migogoro na waandishi wa habari wamezuiwa kufika huko, na hivyo kufanya kuwa vigumu kuthibitisha madai hayo.
Lakini katika ujumbe wa Twitter iliyochapishwa siku ya Jumamosi, ofisi ya Abiy ilisema ameelekea tena katika uwanja wa vita na vikosi chini ya uongozi wake vimeteka maeneo kadhaa ya kimkakati huko Afar na Amhara ikiwa ni pamoja na miji ya Arjo, Fokisa na Boren.
Vita nchini Ethiopia vilianza Novemba 2020 wakati Abiy alipotuma wanajeshi katika eneo la kaskazini mwa Ethiopia la Tigray kuiangusha TPLF baada ya miezi kadhaa ya mvutano mkali na kundi hilo lililokuwa limetawala siasa kwa miongo mitatu kabla ya kuchukua madaraka.
Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa mapigano hayo yamesababisha zaidi ya watu milioni mbili kuyahama makazi yao huku mamia ya maelfu wakikabiliwa na hali kama za baa la njaa, pamoja na ripoti nyingi za mauaji na ubakaji uliofanya na pande zote mbili.
Vyanzo: AFP/Reuters