1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wahofia ghasia zitaisambaratisha Ethiopia

2 Desemba 2021

Mkuu wa shirika la msaada la Umoja wa Mataifa Martin Griffiths ameonya Ethiopia inakabiliwa na hatari ya ghasia za makundi na kukumbwa na kadhia ya uhamiaji ikiwa mzozo uliodumu kwa mwaka mzima utaenea hadi Addis Ababa.

https://p.dw.com/p/43kuF
Martin Griffiths UN Sonderbeauftragter Jemen
Picha: Getty Images/AFP/S. Stjernkvist

Katika mahojiano na shirika la habari la Ufaransa AFP, Griffiths ameelezea wasiwasi kuhusu uthabiti wa nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 115 na makundi 80 ya kikabila.

Griffiths ameonya kwamba vita katika mji mkuu Addis Ababa na kuongezeka kwa ghasia za kijamii kunaweza kuongeza kasi ya hali hiyo kuwa mbaya zaidi.

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yamekuwa yakishughulikia mahitaji yanayozidi kuongezeka nchini Ethiopia na kuweka mipango ya dharura iwapo mzozo huo utakithiri.

Griffiths amesema kwa mtazamo wake wa kibinadamu, baya zaidi linaloweza kutokea iwapo kutakuwa na ghasia mjini Addis ababa ama machafuko karibu na hapo, ni kuongezeka kwa mzozo wa kijamii kote nchini humo.

Äthiopien Tigray-Krise | Soldaten TPLF
Mwanajeshi mtiifu kwa TPLFPicha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Maeneo makubwa yaliyolengwa yanastahili kuepukwa

Griffiths ameongeza iwapo hilo litatokea, watakabiliwa na hali ambayo haijawahi kushuhudiwa awali ya kusambaratika kwa taifa hilo na kwamba machafuko yanayotokana na hali kama hiyo yatakuwa  mabaya zaidi kuliko yale ambayo yametokea katika miezi 13 iliyopita.

Griffiths amesisitiza kuwa hata mapigano yakikaribia mji wa Addis ababa, maeneo makubwa yaliolengwa yanapaswa kuepukwa ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege na mji huo ulio na idadi ya zaidi ya watu milioni 5 ambapo haitafakariki kuwa na mapigano kama hayo.

Mkuu huyo amesema wasiwasi mkuu ni ghasia hizo kugeuka kuwa za kijamii katika maeneo tofauti ya nchi hiyo tofauti na mzozo kati ya serikali na makundi maalumu.

Shirika la Umoja wa Mataifa, limekadiria kuwa maelfu ya watu wameuawa, milioni mbili kupoteza makaazi yao na mamia kwa maelfu ya wengine kusukumwa katika hali kama za njaa tangu ghasia hizo kuzuka mnamo Novemba 2020.

Mgogoro huo ulianza wakati Waziri Mkuu Abiy Ahmed alipotuma wanajeshi katika eneo la kaskazini la Tigray kupambana na vikosi vya kundi la wapiganaji wa  Tigray  (TPLF)  hatua aliyosema ilikuja kujibu mashambulizi ya wapiganaji hao kwenye kambi za jeshi.

Wapiganaji hao wa TPLF walifanya tena mashambulizi na kutwaa tena sehemu kubwa ya Tigray mnamo mwezi Juni kabla ya kujitanua katika mikoa jirani ya Amhara na Afar.

Abiy kwenda mstari wa mbele kuongoza vita hivyo mwenyewe

Mgogoro huo uligeuka kuwa mkali zaidi mwezi mmoja uliopita, wakati kundi la TPLF lilipodai kuteka miji ya kimkakati kwenye barabara kuu kuelekea mji mkuu.

Lakini wiki iliyopita Abiy alikwenda kuongoza vita hivyo mwenyewe na tangu wakati huo, serikali imedai kuchukuwa udhibiti wa miji kadhaa ikiwa ni pamoja na mji wa Lalibela ambalo ni eneo la turathi ya dunia la shirika la UNESCO .

Äthiopien | Premierminister nimmt an Offensive gegen Rebellentruppen Teil
Abiy akiwa na majeshi ya serikali yake katika uwanja wa mapambanoPicha: Ethiopian Prime Minister's Office//AA/picture alliance

Griffiths amesema wakati Umoja wa Mataifa una nia ya kubakia na kutoa misaada bila kujali, hofu inatanda miongoni mwa wafanyakazi wa kigeni kama wanadiplomasia na wengineo mjini Addis ababa kwamba huenda taifa hilo likashuhudia hali tata ya safari za ndege kama ile iliyoshuhudiwa baada ya Taliban kuiteka Afghanistan mnamo Agosti.

Akiongea na shirika la habari la AFP kabla ya kuzinduliwa kwa wito wa kila mwaka wa msaada wa kibinadamu kwa jumuiya ya kimataifa, Griffiths alisema kuwa  karibu dola bilioni 3 zilizoombwa kushughulikia mahitaji ya misaada nchini Ethiopia mwaka ujao ni nyingi kuliko misaada iliyopita kwasabbau ya uwezekano wa mahitaji hayo kuongezeka.