1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tobore Ovuorie atunukiwa tuzo ya DW ya Uhuru wa kujieleza

3 Mei 2021

Tuzo ya uhuru wa kujieleza inayotolewa na shirika la habari la Ujerumani la Deutsche Welle ya mwaka huu ametunukiwa mnaijeria Tobore Ovuorie, anaeripoti habari za uchunguzi, anayepigania kutoa sauti za wale wasiosikika.

https://p.dw.com/p/3ssUl
Freedom of Speech Award 2021 | Preisträgerin Tobore Ovuorie aus Nigeria
Picha: Elvis Okhifo/DW

Tobore Ovuorie anapokumbuka aliyoyapitia miaka saba iliyopita, machozi humbubujika. Yeye kama mwandishi wa habari za uchunguzi alijigeuza na kujifanya kahaba kwa miezi saba, ili kuchunguza mitandao ya biashara za ukahaba nchini Nigeria.

Alipoombwa na mhariri wake kuandika makala kuhusu biashara ya ukahaba, aliona kuna umuhimu wa yeye mwenyewe kujifanya kahaba, ili aweze kujua kila kinachoendelea katika biashara hiyo.

Soma zaidi: Uhuru wa kujieleza: DW yawatuza waandishi

Nia hiyo ilisababishwa pia na rafiki yake wa karibu, aliyeambukizwa virusi vya ukimwi baada ya kusafirishwa kwenda ulaya kufanya ukahaba. Rafiki yake huyo pamoja na wanawake wengi ambao ni wahanga wa usafirishwaji kutoka Nigeria kwenda Italia kila mwaka, ndio walimfanya Bi Ovuorie kufanya uchunguzi huo.

Aliingia katika biashara hiyo ya ukahaba kwa muda wa miezi saba na kubadilisha utambulisho wake, nguo, nywele, pamoja na jinsi anavyoongea. Kwanza kabisa alimpata kuadi (pimp) wa kwanza mjini Lagos na baada ya hapo mjini Abuja. Baadaye ilibidi asafirishwe kwenda Italia akiwa pamoja na wasichana wengine. Katika safari ya kwenda Italia ilibidi wapitie nchini Benin na huko ndio aliweza kutoroka kwa kusaidiwa na wenzake.

ujasiri wa Ovuorie kuripoti mambo yaliyojificha ndio uliompa tuzo hiyo

DW Freedom of Speech Award 2021 für Tobore Ovuorie
Tuzo ya uhuru wa kujieleza 2021 aliyokabidhiwa Tobore OvuoriePicha: DW

Wakati alipojifanya kahaba alinyanyaswa kingono, pamoja na kupigwa nusuru ya kuuliwa. Pia alishuhudia watu waliokuwa wakichinjwa na kutolewa vioungo muhimu vya mwili kwa ajili ya kuuzwa kwenye masoko myeusi. Ingawa mambo aliyoyashuhudia yamemletea msongo wa mawazo, Tobore Ovuorie anaona kwamba kazi yake ya uandishi wa habari za uchunguzi ndio inayomfaa mpaka sasa.

Soma zaidi: DW yamtunukia Anabel Hernández tuzo ya Uhuru wa Habari

"Hiki ndio kitu ambacho nimeamua kukifanya katika maisha yangu yote. Nimeamua kusimama kwa ajili ya wale wasio na sauti kwa kutumia nguvu za maandishi. Hiyo ndio maana naona kazi ya uhandishi wa habari za uchunguzi ndio inayonifaa kabisa."

Mkurugenzi Mkuu wa Deutsche Welle, Peter Limbourg, alisema ni ujasiri huo wa kuripoti mambo yaliyojificha katika jamii, ndio umemfanya Tobore kupewa tuzo ya uhuru wa kujieleza ya DW. 

"Nadhani yeye ni mwanamke jasiri na nafikiri tuzo kama hiyo itamsaidia katika kazi zake na natumaini pia itasaidia kumwongezea ulinzi wake," alisema  Peter Limbourg. 

Tuzo hiyo ya uhuru wa kujieleza ya Deutsche Welle ilianzishwa mwaka 2015 na inanuia kuwatambua waandishi wa habari au harakati mbali mbali zinazokuza uhuru na haki ya kujieleza.

Mwandishi: Harrison Mwilima/DW