Tinubu aahidi kushughulikia madai ya raia
5 Agosti 2024Kiongozi huyo wa Nigeria amesema mikutano ya kampeni imegeuka na kuwa ya vurugu akiwalaumu watu wachache wenye ajenda ya kisiasa kwamba ndio wanaochochea maandamano hayo.
Licha ya wito huo, maandamano hayo bado yanaendelea katika maeneo machache, ikiwa ni pamoja na mji wa Lagos ambao ni kitovu cha uchumi nchini Nigeria.
Soma zaidi: Watu 13 wauawa katika siku ya kwanza ya maandamano Nigeria
Rais Tinubu katika hotuba yake ya kwanza kwa umma juu ya maandamano hayo amesema anaelewa machungu na mfadhaiko uliosababisha watu kandamana, lakini amewahakikishia Wanaigeria kwamba serikali yake imejitolea kusikiliza na kushughulikia wasiwasi wa wananchi.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeripoti vifo vya waandamanaji tisa katika makabiliano na polisi, na watu wengine wanne waliouawa kwa bomu. Hata hivyo, polisi wa Nigeria wameikanusha ripoti hiyo ya Amnesty International.