Tigray yajikongoja kuelekea amani mwaka mmoja baada ya vita
2 Novemba 2023Kabla ya kuzuka kwa vita kati ya Jeshi la Ulinzi la Taifa la Ethiopia (FDRE) na Vikosi vya Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF, miaka mitatu iliyopita, Haftom Kidai, 25, hakuwa na uzoefu wa kijeshi, hakuwahi kubeba bunduki, na alikuwa akijishughulisha na biashara binafsi.
"Baada ya vita kuanza, vikosi vya Ethiopia na Eritrea viliingia Tigray na kuanza kufanya ukatili. Hapo ndipo nikajiunga na mafunzo ya kijeshi na kuanza kupambana kama ilivyokuwa kwa vijana wengi wa Tigray," Haftom aliiambia DW.
Haftom alijeruhiwa vibaya kwenye uwanja wa vita. Sasa, nusu ya mwili wake umepooza na anaishi katika kituo cha malezi cha jeshi katika mji mkuu wa Tigray, Mekelle.
Hakuna matibabu sahihi kwa maveterani
Licha ya mateso yake yote, kijana huyo hana kinyongo. "Nilijiunga na mapambano kwa ajili ya nchi yangu, kwa ajili ya watu wangu, kwa ajili yangu mwenyewe. Sijutii kujitolea kwangu. Nilifanya nilichopaswa kufanya," alisema Haftom.
"Lakini sasa, sisi sote hapa, nikiwemo mimi mwenyewe, tumekuwa walemavu. Tuna mahitaji mengi. Jambo kuu ni kwamba nataka kupata matibabu. Nikipata matibabu sahihi, sitaki kitu kingine chochote."
Soma pia: Baraza jipya la mawaziri la utawala wa mpito wa Tigray
Waethiopia wengi walipata hasara kubwa wakati wa vita vya kikatili vilivyoanza Novemba 2020. Vilidumu kwa miaka miwili na kuua takriban watu 600,000, kulingana na Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, mpatanishi mkuu wa amani wakati wa mzozo huo.
Wengi zaidi walijeruhiwa. Zaidi ya hayo, Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa mapigano yalisababisha karibu watu milioni 1.7 kukimbia makazi yao na kusababisha athari za kimwili na kisaikolojia kwa mamilioni ya watu wa Tigray kama Haftom.
Mazungumzo na pande zote mbili zinazopigana yaliongozwa na Umoja wa Afrika, katika mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria, ambapo vikosi vya kikanda kutoka Tigray na serikali ya Ethiopia, vilisaini makubaliano ya usitishaji mapigano ya kudumu Novemba 3, 2022. Hatimaye, makubaliano ya amani yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ethiopia.
Maisha yarejea taratibu Mekelle
Baada ya makubaliano ya amani, sio tu milio ya risasi ilikoma, lakini serikali pia iliondoa mzingiro uliokuwa umewekwa dhidi ya Tigray.
Mawasiliano ya simu, intaneti, usafiri, shughuli za kibiashara, na utoaji wa misaada ya kibinadamu, uliositishwa kwa miaka miwili, vilianza tena baada ya kusainiwa kwa mkataba wa amani.
Soma via: Ethiopia yaondoa mashtaka dhidi ya viongozi wa Tigray
Polepole, mji mkuu wa Tigray, Mekelle, ulianza kupata uhai baada ya kumalizika kwa vita. Wakazi wa mji huo pia wanaonekana kufurahia amani. Bilen Mitiku, mkazi wa Makelle, aliiambia DW kwamba kutoweza kusikia milio ya risasi, ndege za kivita au droni kumekuwa baraka.
Kulingana na Mitiku, baada ya makubaliano ya amani, Tigray inaonekana kuwa wazi zaidi kwa ulimwengu katika masuala ya mawasiliano na usafiri.
Mahitaji ya kiutu bado ni changamoto
Hata hivyo, mwaka mmoja baada ya makubaliano ya amani, bado kuna mambo mengi yanayotatiza, alisisitiza Mitiku. "Mengi bado hayajabadilika, mengi yamesalia gizani, muhimu zaidi, ndugu zetu waliokimbia makazi yao. Wamekuwa mbali na nyumbani kwao karibu miaka minne sasa."
Mashirika ya Kimataifa ya misaada bado yanajitahidi kusaidia watu wanaohitaji. Ukame, kipindupindu na milipuko ya malaria, bila kusahau tauni ya nzige, vilisababisha madhara zaidi na kuzidisha hali mbaya.
Kulingana na ofisi ya uratibu wa masuala ya kiutu ya Umoja wa Mataifa, OCHA, hali ya kiutu inasalia kuwa tete. Zaidi ya watu milioni moja wanakadiriwa kuendelea kuwa wakimbizi wa ndani na wengine milioni 1.5 huenda wakahitaji msaada wa chakula.
Zaidi ya hapo, Umoja wa Mataifa umeonya juu ya ukatili unaoendelea, ikiwemo uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Soma pia:Utafiti wabaini vifo 1,329 kutokana na njaa katika mkoa wa Tigray nchini Ethiopia
Daniel Semungus, mhadhiri wa chuo kikuu cha Mekelle, aliiambia DW kuwa maadhimisho ya mwaka wa kwanza wa makubaliano ya Pretoria yana hisia mseto na za kipekee miongoni mwa watu wa Tigray.
"Mateso ya wakimbizi wa ndani yanaendelea kutuathiri sote," Semungus alisema, na kuongeza kuwa kuna hatua fulani zimepigwa.
"Mawasiliano, Intaneti imerejeshwa. Watoto wanakwenda shule, watu wanaweza kuvikifia vituo vya huduma za afya na kumekuwepo na urejeshaji wa aina zote za usafiri.
Licha ya hayo, watu wengi mkoani Tigray wanaendelea kudai utekelezaji kamili wa makubaliano ya amani yaliosainiwa mwaka mmoja uliyopita.
Mgogoro huo ulimhamisha Hagos Tesfay, ambaye sasa anaishi katika wilaya ya Irob ya Tigray, inayopakana na Eritrea. Jumuiya yake iko chini ya udhibiti wa jeshi la Eritrea, aliiambia DW.
"Tangu kusainiwa kwa makubaliano ya amani huduma kama vile benki, mawasiliano ya simu na umeme, ambazo zilifungwa katika maeneo mengi ya Tigray, zimefunguliwa. Lakini katika wilaya ya Erob, hakuna kilichobadilika. Sehemu kubwa ya wilaya ya Erob bado inadhibitiwa na Jeshi la Eritrea," Hagos alisema.
Makubaliano ya amani hayajatekelezwa kikamilifu
Gebreselassie Kidane alifurushwa kutoka zoni ya Tigray Magharibi, eneo ambalo sasa liko chini ya udhibiti wa wanamgambo wa Amhara. "Miaka mitatu iliyopita vita vilipoanza tulitoka nje ya nyumba zetu na kuokoa maisha yetu, lakini maisha yetu hapa ni magumu hakuna huduma za msingi hakuna msaada,” alisema Kidane.
Aliiambia DW kwamba hata baada ya vita kuisha, hawakuweza kurudi nyumbani kwao.
Soma pia: Ethiopia yaondoa hali ya hatari mapema, ikisema vita vimetulia
Muungano wa Mashirika ya Kiraia ya Tigray (ACSOT) unadai kuwa mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka mmoja uliopita haujatekelezwa kikamilifu. "Serikali ya shirikisho haifanyi vya kutosha kutimiza ahadi zake," Yared Berha, mkuu wa Chama cha Kiraia cha Tigray, aliiambia DW.
Redaei Halefom, mkuu wa mawasiliano katika utawala wa mpito wa Tigray, aliitaka serikali kuchukua jukumu la uondoaji wa vikosi vya kigeni kutoka Tigray na kurejea mara moja kwa raia waliohamishwa kutokana na vita.
"Tunatarajia serikali ya shirikisho kuwaondoa wanamgambo wote kutoka kwa Jeshi la Ulinzi la Ethiopia huko Tigray," Redaei alisema.
Alisisitiza kuwa kwa mujibu wa makubaliano hayo, wanamgambo wa Amhara na wanajeshi wa Eritrea wanapaswa kuondoka Tigray.