Baraza jipya la mawaziri la utawala wa mpito wa Tigray
6 Aprili 2023Baraza hilo jipya la mawaziri la Tigray lina watu 27, ambao linajumuisha wanachama wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF, na makamanda wa kijeshi ambao walipigana na vikosi vya serikali wakati wa vita kwenye jimbo hilo.
Jenerali Tadesse Worede, kamanda wa vikosi vya TPLF wakati wa vita, ameteuliwa kuwa makamu wa kwanza wa rais wa jimbo la Tigray, mwenye dhamana ya amani na usalama. Na makamu wa pili wa rais katika baraza hilo la mawaziri ni Tsadkan Gebretensae, ambaye alikuwa mkuu wa majeshi ya Ethiopia katika miaka ya 1990 na 2000 wakati TPLF ilipotawala serikali kuu na baadae kuwa mwanamkakati mkuu wa vikosi vya TPLF wakati wa vita vya Tigray. Tsadkan amepewa dhamana ya demokrasia na utawala bora.
Kuanzishwa kwa utawala wa mpito ilikuwa moja ya vipengele muhimu vya mkataba wa amani uliotiwa saini katika mji mkuu wa Afrika Kusini Pretoria mwezi Novemba 2022 kati ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed na Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF.
Ethiopia yawaondolea mashtaka viongozi wa TPLF
Wiki mbili iliyopita, serikali ya Ethiopia ilimteuwa Getachew Reda, msemaji wa TPLF, kuwa mkuu wa serikali ya mpito ya jimbo la Tigray. Hatua hiyo ilifuatiwa na ile ya bunge la Ethiopia kukiondoa chama cha TPLF katika orodha rasmi ya makundi ya kigaidi kwa mujibu wa makubaliano ya mwezi Novemba.
Debretsion Gebremichael, ambaye alikuwa rais wa Jimbo la Tigray tangu 2018, alikabidhi rasmi hatamu ya uongozi kwa Getachew wakati wa hafla ya jana Jumatano. Gebremichael aliwahimiza wajumbe wa utawala wa mpito wa Tigray, kuchangia katika kudumisha amani, usalama na maslahi ya watu wa Tigray.
Pongezi za kimataifa
Mgogoro wa Tigray ulianza Novemba 2020 pale Waziri Mkuu Abiy Ahmed alipoyatuma majeshi ya serikali kuu kuuangusha uongozi wa TPLF akiwashutumu wapiganaji wake kwa kushambulia kambi za kijeshi za serikali ya shirikisho.
Wiki hii, Umoja wa Ulaya na Marekani zilipongeza hatua iliofikiwa nchini Ethiopia. Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell aliahidi kwamba watarejesha mahusiano ya kawaida na serikali ya mjini Addis Ababa hatua kwa hatua.