Ethiopia yasema hakuna tarehe ya kurejesha intaneti Tigray
30 Novemba 2022Waziri wa ubunifu na teknolojia wa Ethiopia Belele Molla, amesema urejeshaji wa huduma za intaneti katika mkoa wa Tigray utakwenda sambamba na urejeshaji wa huduma za simu na umeme, lakini hakuna tarehe makhsusi iliyowekwa kwa malengo hayo.
Balele amesema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa kuhusu usimamizi wa intaneti, unaofanyika wiki hii mjini Addis Ababa.
Tigray, ambako ni nyumbani kwa watu milioni tano, imekosa huduma za intaneti, simu na benki tangu kuzuka kwa vita kati ya jeshi la serikali ya shirikisho na vikosi vinavyoongozwa na chama cha Ukombozi wa watu wa Tigray, TPLF, Novemba 2020.
Mapatano ya kusitisha mapigano kati ya pande hasimu yaliofikiwa nchini Afrika Kusini mapema mwezi huu, yanaitaka serikali kurejesha huduma za msingi za Tigray, lakini uzimaji wa wa mawasiliano bado unaendelea.
-