1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUturuki

Tetemeko jipya la ardhi latikisa Uturuki na Syria

21 Februari 2023

Watu watatu wamefariki dunia na mamia kujeruhiwa kufuatia tetemeko jipya la ardhi ambalo limetikisa Uturuki na Syria usiku wa kuamkia Jumanne.

https://p.dw.com/p/4Nlyl
Türkei | Erneutes Beben in der Provinz Hatay
Picha: REUTERS

Mkasa huo unajiri mnamo wakati nchi hizo zikikabiliwa na athari ya matetemeko mawili mabaya ya ardhi yaliyotokea wiki mbili zilizopita na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.

Taarifa za awali punde baada ya tetemeko jipya la ardhi kuripotiwa katika mkoa wa Hatay nchini Uturuki zilieleza kuwa watu wasiopungua watatu wameuawa na zaidi ya 200 walijeruhiwa na walikimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Waziri wa mambo ya ndani nchini Uturuki Süleyman Soylu amesema hayo baada ya matetemeko mawili kutokea. Tetemeko la kwanza liliripotiwa kuwa na ukubwa wa 6.4 kwenye vipimo vya ritcha na la pili lililotokea dakika tatu baadaye, nalo lilikuwa na ukubwa wa 5.8 kwenye vipimo vya ritcha. Hayo ni kulingana na mamlaka ya Uturuki inasimamia majanga (AFAD).

Shirika la Uturuki linalofuatia matetemeko ya ardhi nchini Kandili, limesema kitovu cha tetemeko la hivi karibuni ni wilaya ya Samandag Uturuki.

Mwili wa Atsu warejeshwa Ghana kutoka Uturuki

Matetemeko hayo ya ardhi yametikisa hadi maeneo ya Syria, Israel, Iraq, Lebanon na Palestina. Hayo ni kulingana na ripoti za vyombo vya habari katika nchi hizo.

Jamaa asikitika baada ya tetemeko jingine la ardhi kutikisa Antakya jimbo la Hatay Uturuki Februari 20, 2023.
Jamaa asikitika baada ya tetemeko jingine la ardhi kutikisa Antakya jimbo la Hatay Uturuki Februari 20, 2023.Picha: Clodagh Kilcoyne/REUTERS

Watu watahadharishwa dhidi ya kuingia majumbani

Soylu amewatahadharisha watu wasiingie majumbani akisema kumekuwa na zilizala 26 za baada ya matetemeko hayo.

Katika taifa jirani la Syria, watu wasiopungua 470 walijeruhiwa baada ya matetemeko hayo. Watu 150 walijeruhiwa katika jimbo linalodhibitiwa na waasi, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Shirika la haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza White Helmets, limesema takriban watu 320 wamejeruhiwa katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali. Limeongeza kuwa wengi wa waliojeruhiwa waliteguka na kuvunjika viungo au walikwaruzwa mwilini.

Blinken akutana na Rais Erdogan katika ziara yake Uturuki

Mkuu wa shirika hilo Raed Saleh ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba majeraha mengi yalisababishwa kwa sababu watu waliingiwa woga na taharuki na kusababisha wengine kuruka kutoka majengo ya ghorofa wakijaribu kujinusuru. Katika visa vingine watu walizirai.

Shule zafungwa Beirut

Katika mji wa Beirut nchini Lebanon, waziri wa elimu ameamuru shule, na vyuo vyote vya masomo kufungwa Jumanne baada ya tetemeko hilo lililotikisa mji huo pia.

Abdel Kafi ambaye ni mwanaharakati wa haki za binadamu kaskazini magharibi mwa Syria amesema tetemeko hilo lilikuwa kubwa kama la hapo awali ila halikudumu kwa muda mrefu.

Matetemeko hayo ya hivi karibuni, yamejiri wiki mbili baada ya matetemeko mabaya ya ardhi yaliyotokea Uturuki na Syria na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 47,000.

(Chanzo: DPAE)