1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwili wa Atsu warejeshwa Ghana kutoka Uturuki

20 Februari 2023

Mwili wa winga wa Ghana Christian Atsu umewasili mjini Accra, siku moja baada ya kupatikana akiwa amekufa kwenye jengo lililoporomoka kusini mwa Uturuki kufuatia tetemeko kubwa la ardhi

https://p.dw.com/p/4NkhH
Fußball | Christian Atsu
Picha: Scott Heppell/REUTERS

Atsu alikuwa hajulikani aliko tangu tetemeko la ardhi la Februari 6 kufuatia kuporomoka kwa jengo alimokuwa akiishi mjini Hatay. Alikuwa na umri wa miaka 31. Jeneza lililokuwa limefunikwa bendera ya taifa ya Ghana lilipokelewa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kotoko na Makamu wa rais Mahamudu Bawumia na guaride kubwa la kijeshi

"Ni siku ya huzuni kubwa ambayo tupo hapa kuupokea mwili wa ndugu yetu, mtoto wetu, mume wetu, mjomba wetu. Mkasa uliotokea Uturuki karibu wiki moja iliyopita lilikuwa janga kubwa. Na tulisubiri na kusali kwa hamu na hofu kubwa kuwa ndugu yetu Christian Atsu angepatikana akiwa hai."

Atsu alikuwa amepangiwa kuondoka kusini mwa Uturuki saa chache tu kabla ya tetemeko hilo lakini meneja wa klabu ya Hatayspor alisema Ijumaa kuwa Mghana huyo aliamua kubaki na wenzake wa klabu hiyo baada ya kufunga bao la ushindi katika mechi ya ligi kuu mnamo Februari 5. Alijiunga na Hatayspor Septemba mwaka jana baada ya kuchezea vilabu vya Everton, Chelsea na Newcastle United katika Premier League ya England.

reuters