Tebogo wa Botswana nusra aibuke bingwa wa dunia
21 Agosti 2023Letsile Tebogo wa Botswana aliinyakulia nchi yake na bara zima la Afrika medali ya fedha ambayo ndiyo medali ya kwanza ya Afrika katika mita 100 kwenye historia ya mashindano hayo.
Tebogo aliweka rekodi ya kitaifa kwa kukimbia kwa sekunde 9.88 na alikuwa na haya ya kusema baada ya mbio hizo.
"Naifurahia sana medali ya fedha na kwetu sisi, ni ufanisi wa ziada kwasababu lengo kuu lilikuwa kufika fainali tu, kwa hiyo kushinda medali ni jambo bora zaidi kwangu na kocha wangu," alisema Tebogo.
Ferdinand Omanyala wa Kenya ambaye ndiye bingwa wa Jumuiya ya Madola na bingwa wa Afrika pia, alimaliza katika nafasi ya saba.
Omanyala anasema hafahamu kilichotokea ila alihisi mwili wake hauendi kwa kasi aliyotaka. Bingwa mtetezi Fred Kerley wa Marekani hakufuzu fainali hiyo hivyo hakuweza kulitetea taji lake.
Chanzo: DPAE/APE/Reuters