1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tawala za Kifalme zajiimarisha barani Ulaya

20 Januari 2024

Katika nchi kadhaa barani Ulaya, Wafalme na Malkia wanaendelea kutawala. Tawala hizi zinaendelea kuimarika licha ya mataifa kadhaa kufanya mabadiliko kuelekea demokrasia, lakini baadhi ya wafalme bado wana utawala kamili

https://p.dw.com/p/4bUzO
Malkia wa Denmark Margarethes alimkabidhi uongozi mwanaye Mfalme Frederik X
Mfalme wa Denmark Frederik X akiwa na mkewe Malkia Mary wakisalimia umati wa watu kutoka Kasri la Christiansborg mjini Copenhagen, Denmark:14.01.2024Picha: Martin Meissner/AP Photo/picture alliance

Karibu asilimia 22 ya nchi zote ulimwenguni hutawaliwa na uongozi wa kifalme. Hii ikiwa ni sawa na nchi 43 kati ya 194 yanayotambuliwa rasmi. Mbali na Ulaya, tawala za kifalme zinapatikana barani Afrika, Mashariki ya Kati, Asia na huko Caribbean.

Tawala nyingi za kifalme zilianza tangu enzi himaya ya Uingereza (British Empire) , na mfalme wa Uingereza bado ni mkuu wa nchi karibu 14 nje ya bara la Ulaya, ikiwa ni pamoja na Canada na Australia.

Taifa moja la kifalme miongoni mwa saba yanayotawala barani Ulaya, limefanya mabadiliko ya uongozi. Baada ya Uholanzi na Ubelgiji mnamo mwaka 2013, Uhispania mwaka 2014 na Uingereza mwaka 2022, sasa ilikuwa zamu ya Denmark ambapo Malkia Margarethe II mwenye umri wa miaka 83 amekabidhi kijiti cha enzi kwa mtoto wake Frederik siku ya Jumapili ya Januari 14 mwaka 2023, baada ya miaka 52 madarakani.

UK Walinzi wa Kasri la Kifalme la Buckingham
Walinzi wa Kasri la Kifalme la Buckingham mjini London Uingereza:11.09.2022Picha: Stuart Brock/AA/picture alliance

Taarifa hii ya kushangaza kutoka kwa familia ya kifalme ya Denmark inafuata utaratibu uliopo. Mbali na  Uingereza, wafalme wengi wa Ulaya hawapendi kufa wakiwa bado wako madarakani. Badala yake, hustaafu na kuachia nafasi hiyo kwa watoto wao. Akiwa na umri wa miaka 55,  Mfalme Frederik wa Denmarkametumia muda mrefu wa maisha yake kujiandaa kukalia kiti hicho.

Soma pia:Mfalme Charles III aahidi kufuata nyayo za mamake

Yeye na mke wake Mary raia wa Australia, tayari wamefanikiwa kupata watoto ambao ndio warithi wa Ufalme huo mkongwe zaidi barani Ulaya. Raia wa Denmark wanaonekana kufurahishwa na utawala wao huku kura za maoni zikibainisha kuwa asilimia 80 ya Wadenmark wameridhika na mtawala wao.

Wanaotarajiwa kuchukua uongozi hapo badaye ni Mwanamfalme Victoria wa Sweden na Mwanamfalme Haakon wa Norway. Victoria anajiandaa kuchukua nafasi ya baba yake, Carl XVI Gustaf, ambaye ametawala kwa zaidi ya miaka 50. Haakon atachukua nafasi ya baba yake King Harald V mwenye umri wa miaka 86, ambaye amekuwa akionekana mara chache hadharani kutokana na matatizo yake ya kiafya.

Rais Macron wa Ufaransa pia ni Mwanamfalme

Utawala wa Kifalme  Andorra
Emmanuel Macron sio tu rais wa Jamhuri ya Ufaransa kwa sasa, lakini pia ni mkuu katika taifa la kidemokrasia la Andorra.Picha: Batard Patrick/ABACA/picture alliance

Kwa ujumla barani Ulaya, watawala wa kifalme huwa na majukumu yasiyo ya kimamlaka na yenye ushawishi mdogo kisiasa. Hali hii hushuhudiwa katika utawala wa kifalme wa Luxembourg na Liechtenstein, pamoja na Monaco licha ya kuwa Mwanamfalme Albert II ana ushawishi mkubwa.

Soma pia: Mkuu wa kundi la watu wanaopinga ufalme nchini Uingereza Graham Smith ameachiwa huru.

Katika taifa dogo la Andorra, lililo katikati ya bonde la Ufaransa na Uhispania, limekuwa likiongozwa na viongozi wenza wawili ambao ndio huchukuliwa kama wakuu wa nchi. Kiongozi mmoja ni askofu wa Uhispania wa huko Urgell na mwingine ni rais wa Ufaransa. Hii ina maana kwamba Emmanuel Macron sio tu rais wa Jamhuri ya Ufaransa kwa sasa, lakini pia ni mkuu katika taifa la kidemokrasia la Andorra.

Vatican: Ufalme wa Ulaya usiorithishwa

Vatican Papa Francis akiongoza ibada ya mwaka mpya wa 2024
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ambaye pia ni Kiongozi wa Vatican( Aliye katikati) akiongoza ibada ya mwaka mpya: 01.01.2024Picha: Andrew Medichini/AP photo/picture alliance

Utawala pekee barani Ulaya ambao waweza kuchukuliwa kama wa kifalme ambao kiongozi wake huchaguliwa na si kurithishwa ni Vatican. Papa Francis sio tu anaongoza Kanisa Katoliki, lakini pia ndiye mtawala kamili wa taifa dogo zaidi ulimwenguni la Vatican.

Mwanahistoria wa Chuo Kikuu cha Potsdam na mtaalam wa familia za kifalme Monika Wienfort anadhani raia wengi wa mataifa ya kifalme wanaridhishwa na viongozi wao. Bi Wienfort amesema kuwa hakukuwa na juhudi kubwa za kusitisha aina hii ya utawala katika falme za barani Ulaya. Amesisitiza kuwa vitendo vya kujiuzulu na kurithi nafasi hizo vimefanyika bila matatizo makubwa mbali na maandamano kadhaa ya makundi ya watu wanaopinga tawala za kifalme.

Soma pia: Mfalme Charles III wa Uingereza aanza ziara Ujerumani

Wienfort ameendelea kuwa utawala wa kifalme umedumu barani Ulaya katika mataifa ambayo hayakushuhudia mapinduzi kama yaliyotokea Ufaransa, Italia, Austria na Ujerumani. Tawala za kifalme barani Ulaya zinahusiana kwa njia moja ama nyingine, na familia za watu maarufu na tajiri wa Ujerumani.

Tawala za kifalme hustawi kwa kuendeleza mila lakini pia kutokana na taarifa za udaku na kashfa kuhusu maisha ya wanafamilia hao. Mwanamfalme Charles wa Uingereza aliwahi kusema mnamo mwaka 2008 kuwa maisha ya familia yake ni sawa na tamthilia. Baba yake Philip, wakati mmoja aliielezea kasri la Windsor kuwa kama kampuni iliyopewa jukumu la kuzalisha filamu nzuri kwa malipo ya pesa za walipa kodi.