Tanzania yarejea nyumbani, Kenya bado yasubiri
2 Julai 2019Wakati Tanzania ikichezea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Algeria, Kenya nayo ilikuwa ikikaangwa bila mafuta na Senegal na kukubali kipigo kama hicho cha mabao 3-0. Wakati Tanzania ambayo haina pointi hata moja kutokana na michezo mitatu , ikifunga vifago na kurejea nyumbani , hatima ya Kenya bado haijaamuliwa , kutokana na kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Tanzania wiki iliyopita. Kenya pamoja na Afrika kusini sasa zinasubiri michezo ya makundi kumalizika leo kuona iwapo ni miongoni mwa timu nne bora zilizoshindwa ili kufuzu kuingia katika duru ya mtoano ya timu 16 zilizosalia.
Afrika kusini iliyokuwa katika kundi D ilifungwa bao 1-0 na Morocco jana jioni , wakati Nambia ilikubali kipigo cha mabao 4-1 dhidi ya Cote D'Ivoire.
Michezo ya leo ni ya makundi E na F ambapo Benin yenye pointi 2 itapambana na Cameroon ambayo imefikisha pointi 4, ikiwa inaoongoza kundi hilo. Guinea Bissau yenye pointi 1 tu kutokana na michezo miwili inaumana na Ghana ambayo katika mashindano ya mwaka huu imeonekana kusua sua na hadi sasa ina pointi 2 tu sawa na Benin. Baada ya mapambano hayo kundi E litaingia uwanjani kuoeshana kazi, wakati Angola ambayo hadi sasa imejinyakulia pointi 2 , itaingia dimbani kuoneshana kazi na Mali yenye pointi 4 na inaongoza katika kundi E. Mauritania ambayo ndio mara yake ya kwanza kufuzu katika mashindano haya ya kombe la mataifa ya Afrika katika historia ya nchi hiyo inaumana na Tunisia.
Algeria haikuwateremsha majogoo wake 11 waliopambana na Senegal katika mchezo wa kwanza na kushinda wiki iliyopita lakini waliweza pia kuishinda Tanzania kwa mabao 3-0 mjini Cairo jana na kuchukua usukani wa kundi C wakiwa na pointi 9. Hii ina maana kwamba Algeria imeshinda michezo yake yote mitatu katika kundi hilo, wakati Tanzania ndio timu pekee dhaifu ambapo imepoteza michezo yake yote mitatu, ikirejea mjini Dar es Salaam bila pointi na mzigo wa mabao manane wakati yenyewe ikizifumania nyavu mara mbili tu.
Senegal inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi sita, Kenya ikichukua nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 3, na Tanzania ikirejea kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo baada ya kukosekana kwa muda wa miaka 39 , ikiambulia patupu na nafasi ya nne.
Kufuzu kwa Senegal jana kunaongeza idadi ya timu ambazo tayari zimekwisha fuzu kuingia katika awamu ya mtoano kufikia timu 12, awamu inayoanza rasmi siku ya Ijumaa.
Wenyeji Misri , Madagascar ambayo imemshangaza kila mpenzi wa kandanda hadi sasa , Algeria na Morocco zinasonga mbele kama washindi wa makundi yao na Uganda, Nigeria, Senegal na Cote D'Ivoire zimeingia katika awamu hiyo kama timu zilizoshika nafsi ya pili.
Guinea na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo zimefuzu kuingia katika duru ya mtoano kwa njia ya kuwa timu bora zilizoshindwa.