Tanzania yafungia mitandao ya gazeti la Mwananchi
3 Oktoba 2024Hatua ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya kusimamisha kwa muda leseni ya kampuni ya habari ya Mwananchi Communications Ltd(MCL) imetafsiriwa tofauti na wadau wa Habari Tanzania, ambao wameikosoa kanuni ya maudhui mtandaonina kusema inaacha mwanya wa tafsiri tofauti.
Mwanahabari Mkongwe nchini hapa Kajubi Mukajanga, amesema maudhui hayo hayakulenga kumuudhi yeyote ispokuwa yalilenga kuonesha tatizo lililopo nchini.
"Mimi sioni ni tatizo kwasababu hata ngazi za juu wametambua kuwa lipo na kuagiza lifanyiwe kazi, Kajubi aliiambia DW.
Aliongeza kwamba hatua iliyochukuliwa na mamlaka ya mawasiliano nchini ni kujenga hofu kwa umma ikiwemo vyombo vya habari kuhusiana na suala la kutoa maoni.
Soma pia:Samia Suluhu: Serikali si mshindani wa vyombo vya habari
Baraza la Habari nchini humo MCT limesema ni wakati sasa wa tasnia ya habari kuketi na serikali uelewe juu ya umuhimu wa tasnia hiyo katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku.
Mkurugenzi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Ernest Sungura, aliiambia Dw kwamba kuna haja ya vipengele muhimu kujadiliwa ili kuweka mizani sawia "kuna haja ya kukaa meza moja na kufanya upande wa serikali uelewe zaidi, bado makandokando vya kufanya uhuru unakuwa haupo, kuhakikisha kwamba watu wapewe huo uhuru, watu wazingatie maadili."
Hoja za TCRA kwa gazeti la mwananchi
Katika taarifa yake, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) imeeleza kuwa, Oktoba Mosi, kampuni ya Mwananchi ilichapisha maudhui mjongea au audiovisual kwenye mitandao yake ya kijamii, ambayo yamezuiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 16 ya maudhui ya mtandaoni ya mwaka 2020.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mara baada ya kupewa leseni ya maudhui ya mtandaoni, kampuni ya MCL ilitakiwa kutokuchapisha au kutangaza maudhui yaliyozuiwa ikiwa ni pamoja na yanayolenga kudhihaki au kuharibu taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kutokana na kosa hilo, TCRA imesitisha kwa muda leseni ya maudhui mtandaoni kwa kampuni hiyo ya Habari kuanzia jana Oktoba 2 hadi Novemba 2.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Victor Mushi, amekiri kufungiwa kwa mitandao yao ya kijamii X, instagram
Soma pia:Wadau wajadili uhuru wa vyombo vya habari Tanzania
Hata hivyo saa chache zilizopita, Mwananchi ilisambaza taarifa iliyoeleza kuwa tayari kampuni hiyo imeondoa maudhui yaliyochapishwa kwenye mitandao yao.
Katika taarifa hiyo wameeleza kuwa wameondoa maudhui hayo katika mitandao yao ya kijamii ikiwamo Instagram na X kwa kuwa maudhui hayo yanaibua wasiwasi kuhusu ulinzi na usalama wa raia nchini.
Kanuni za maudhui ya mtandaoni za mwaka 2022 zimetengenezwa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta 2010 (Epoca). Madhumuni ya kanuni hizi ni kusimamia na kuendesha maudhui yanayotolewa kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari vya kimtandao.
Hata hivyo wadau wa Habari nchini wamekuwa wakipinga kanuni hizo na kudai kuwa zinaminya uhuru wa Habari