Tangazo la usitishaji mapigano Congo haliaminiki kwa wenyeji
1 Agosti 2024Tangazo la siku ya Jumatano la kusitisha mapigano kati ya Congo na waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wa M23 walioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limepokelewa kwa shingo upande na watu wengi wanaoishi katika maeneo yanakofanyika mapigano. Makubaliano hayo, yaliyofikiwa kupitia upatanishi wa Angola, litaanza kutekelezwa kuanzia siku ya Jumapili.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa siku ya Jumanne ya wiki hii yamepongezwa na Ubelgiji, Ufaransa na Umoja wa Ulaya.
Soma zaidi. Umoja wa Mataifa wathibitisha kuwa jeshi la Rwanda linashirikiana na waasi wa M23
Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres naye hakuwa nyuma katika kutoa pongezi zake kwa hatua hiyo, Nikinukuu maneno yake amesema "Tunatumai makubaliano haya yatasaidia kuweka mazingira ya kupunguza mvutano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda na kuwezesha kurejea salama kwa wakimbizi wa ndani makwao," mwisho wa kumnukuu.
Lakini pamoja na hatua hiyo, bado yapo mashaka ikiwa tangazo hilo la kusitisha mapigano litaheshimiwa itakukumbukwa kuwa hata huko nyuma yalishatangazwa matangazo ya namna hiyo lakini bado mapigano yaliendelea bila kuheshimiwa kwa makubaliano.
Mfano huko Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, ambao kwa sasa umezungukwa na waasi na vitengo vya jeshi la Rwanda, kulikuwa na shauku ndogo ya tangazo hilo.
Soma zaidi. Uganda inaongoza mazungumzo ya amani kati ya pande zinazohasimiana Kongo
Tresor Tonde Mabala, mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha La Sapientia huko Goma. alisema tangazo hili "Haitasababisha chochote," "Kusitishwa kwa mapigano kunamnufaisha adui. Waasi kamwe hawaheshimu maamuzi ya jumuiya ya kimataifa."
Makubaliano ya "usitishaji wa muda " ya wiki mbili yalitangazwa tayari Julai 5 na Marekani na kisha yakaongezwa kwa siku 15 hadi Agosti 3.
Tangazo hilo bado halipewi uzito na wenyeji
Kwa sasa mapigano yamepungua, lakini mashirika yasiyo ya kiserikali yanashuku kwa makundi yenye silaha yanachukua fursa ya hali hiyo kujipanga upya kwa mapigano mapya.
"Makubaliano mara nyingi yanakiukwa na pande zinazohusika kwa sababu katika hatua ya sasa, M23 na jeshi la Rwanda wanaendelea kuimarisha misimamo yao", alisema Georges Katsongo, rais wa jumuiya ya kiraia katika mkoa wa Lubero kaskazini mwa jimbo hilo. ambapo waasi wamezidi kupata nguvu katika miezi ya hivi karibuni.
Soma zaidi. Kongo: Kundi la M23 laua watu watano huko Masisi
"Ninakubali kwamba vita vifikie ukomo, kwa sababu jeshi letu limejionyesha kuwa dhaifu mbele ya adui," alisema Roland Kambale, mkazi wa Mabanga Nord wilayani Goma. "Tunaendelea kupoteza kaka na dada zetu katika vita vyao."
Patrick Paluku,mwanachama wa kundi la shinikizo la Veranda Mutsanga huko Goma ametoa wito kwa watu wa Congo kutokubaliana na tangazo hilo. Nikinukuu maneneo yake anasema "Hatutakubali hili. Tunatoa wito kwa watu wa Congo mashariki kupinga,"Tunaamini kuwa kuanzia Agosti 4, Wazalendo wana haki ya kushambulia adui. Vinginevyo waasi wana hatari ya kusonga mbele,"
Maelfu ya raia wengi mashariki mwa Congo wamegeuka kuwa wakimbizi wa kufuatia mapigano ya M23 na wengi wao hawana matumaini na tangazo lililotolewa la usitishaji wa mapigano kwa muda.
Wengi wakidai hatua hiyo haisaidii na ikiwa wataunga mkono basi vikosi vya wanajeshi wa Rwanda ni lazima viondoke kabisa kwenye vijiji vyao.