Taliban yamzuia mtaalamu wa UN kuingia Afghanistan
22 Agosti 2024Bennett aliteuliwa na Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa mwaka wa 2022 kufuatilia hali ya haki za binaadamu nchini Afghanistan baada ya Taliban kuchukua usukani mwaka uliotangulia.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya serikali ya Taliban Abdul Qahar Balkhi amesema Bennett ameshindwa kupata viza ya kuingia Afghanistan.
Bennett, ambaye hapo awali alisema vitendo vya Taliban dhidi ya wanawake na wasichana vinaweza kuwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu, anahudumu nje ya Afghanistan lakini ameitembelea nchi hiyo mara kadhaa kutafiti hali ya haki za binaadamu.
Soma pia:Wasichana milioni 1.4 wazuiwa kwenda shule za sekondari nchini Afghanistan
Mjumbe huyo amesema katika taarifa kuwa anayachukulia majukumu yake kwa umuhimu mkubwa.
Ameihimiza Taliban kuubatilisha uamuzi wake na kusema kuwa ataendelea kushirikiana na Waafghanistan ndani na nje ya nchi hiyo. Miaka mitatu baada ya kuingia madarakani kufuatia kuondoka kwa wanajeshi wa kigeni, Taliban haijatambuliwa rasmi na serikali yoyote ya kigeni.