1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Syria yaomba mataifa ya Kiarabu kuwekeza nchini humo.

16 Mei 2023

Syria iliyokaribishwa tena ndani ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Arab League, imeyatolea mwito mataifa hayo kuwekeza nchini Syria, ambayo imeaathirika pakubwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/4RRlA
Syria imekaribishwa tena kwenye jumuiya hiyo kama ambavyo bendera yake(ya nne kutoka kushoto) inavyoonekana
Syria ilitengwa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu, Arab League kutokana na hatua kali dhidi ya waandamanaji, 2011.Picha: Ahmed Gomaa/Xinhua/picture alliance

Mwito huo umetolewa na waziri wa uchumi na biashara wa Syria wakati wa mkutano wa masuala ya uchumi nchini Saudi Arabia kabla ya mkutano wa kilele wa Arab League, nchini humo. 

Waziri huyo Mohammed Saher al-Khalil alinukuliwa katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo mapema wiki hii akiwakaribisha wawekezaji nchini Syria na kupigia debe fursa muhimu na mazingira yanayovutia kiuwekezaji. Mkutano huo unafanyika Jeddah, Saudi Arabia.

Hata hivyo, vikwazo vikali vya ncini za magharibi dhidi ya serikali ya rais Bashar al-Assad bado vingalipo na huenda vikayafanya mataifa ya Kiarabu na yenye utajiri mkubwa wa mafuta kujitafakari kwanza kabla ya kukimbilia kuwekeza nchini Syria ama hata kutoa ufadhili wa ujenzi wa taifa hilo lililoharibiwa kwa vita. 

Waziri wa fedha wa Saudi Arabia Mohammed al-Jadaan ambaye pia alizungumza kwenye mkutano huo, aliikaribisha tena Syria kwenye muungano huo wa Arab League akisema ana matumaini kwamba watashirikiana kufikia lengo walilojiwekea.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Syria Faisal Mekdad(kushoto) akizungumza na mwenzake wa Saudi Arabia Waleed El Khereiji alipowasili Jeddah, Aprili 12,2023.
Picha: SAUDI PRESS AGENCY/REUTERS

Syria, mapema mwezi huu ilianzisha mazungumzo ya kikanda na Jordan, Saudi Arabia, Iraq, Misri na Amman, kama sehemu ya mkakati uliokuwa ukiongozwa na matataifa ya Kiarabu wa kusuluhisha mzozo wa Syria. Ikumbukwe kwamba Arab League inayoyakutanisha mataifa 22 ulikubaliana mapema mwezi huu kuirejesha Syria iliyosimamishwa uanachama kwa miezi 12.

Wachambuzi wanasema uwekezaji nchini Syria unaweza kukumbwa na vizingiti hadi pale taifa hilo litakapofikia makubaliano ya kisiasa, pamoja na utatuzi wa masuala mengine muhimu ambayo ni pamoja na mamilioni ya wakimbizi wa Syria, biashara inayoshamiri ya madawa ya kulevya pamoja na makundi ya wanamgambo wa itikadi kali.

Bado haiko wazi iwapo Assad atashiriki katika mkutano wa kilele wa Arab League unaofanyika siku ya Ijumaa, ambao tayari amepata mwaliko rasmi. Lakini siku ya Jumatatu, waziri wa mambo ya nje wa Syria Faisal Mekdad aliwasili mjini Jeddah kuhudhuria mikutano inayoutangulia mkutano huo wa kilele, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la serikali ya Syria, SANA.

Rais wa Syria Bashar al-Assad(kulia) akipeana mikono na rais wa Iran Ebrahim Raisi wakati Raisi alipoitembelea Syria Mei 3,2023
Syria imekuwa katika harakati za kurejesha mahusiano na mataifa yaliyoitenga kwa muda mrefu.Picha: Iranian Presidency/AP

Mekdad aliwaambia waandishi wa habari alipowasili Jeddah kwamba hiyo ni fursa mpya ya kuwaonyesha wenzao kuwa kwa sasa hawatizami yaliyopita, bali wanaganga yajayo. Amesema bado kuna changamoto nyingi ambazo bado wanatakiwa kujadiliana na kuunganisha nguvu za kukabiliana nazo. Changamoto hizo ni pamoja na mzozo kati ya mataifa ya Kiarabu na Israel na mabadiliko ya tabianchi.

Syria ilisimamishwa uanachama wa umoja huo wa Kiarabu kufuatia hatua kali za serikali ya Assad dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakiupinga utawala wake mnamo mwaka 2011. Maandamano hayo, hatimaye yaligeuka na kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha vifo vya mamilioni ya raia.

Saudi Arabia imekuwa muungaji mkono mkubwa wa makundi ya wanamgambo yanayojaribu kumpindua Assad, lakini katika miezi ya karibuni Riyadh imetoa mwito wa mazungumzo na wiki iliyopita mataifa hayo mawili yalikubaliana kufungua upya balozi zao.

Kwenye hotuba yake al-Khalil pia aliyashukuru mataifa ya Kiarabu kwa kuwasaidia wakati taifa hilo lilipopigwa na tetemeko la ardhi mwezi Februari na kusababisha vifo vya watu 6,000.

Mbali na Saudi Arabia, Jordan na Misri pia zimerejesha uhusiano na Damascus, ingawa hatua hiyo inapingwa na Kuwait, Morocco na Qatar, ambayo bado inasalia kuwa muungaji mkono mkubwa wa makundi ya uasi yanayopambana na Assad.