1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Sudan: Guterres atoa wito wa kusitishwa mapigano

21 Aprili 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa pande mbili hasimu nchini Sudan kufikia makubaliano ya usitishaji mapigano kwa muda wa siku tatu wakati wa sikukuu ya Waislamu ya Eid el-Fitr

https://p.dw.com/p/4QNV7
Somalia Mogadischu Besuch UN-Generalsekretär Guterres
Picha: FEISAL OMAR/REUTERS

Hali bado si shwari nchini Sudan ambako mapambano ya kuwania udhibiti wa miji na maeneo muhimu ya nchi yanaendelea kati ya vikosi tiifu kwa mkuu wa majeshi ambaye pia ni mtawala mkuu wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na vile vinavyomtii naibu wake Mohammedi Hamdan Dagalo, maarufu kama Rapid Support Forces, RSF.

Kwa siku ya saba mfululizo vikosi vya Al-Burhan na vile vya Dagalo vimeendeleza mapigano makali. Maelfu ya raia wamelazimika kuondoka katika mji mkuu Khartoum wakati milio ya risasi na milipuko ya mabomu vikiendelea kusikika sehemu mbalimbali za jiji hilo. Idadi kubwa ya watu walivuka mpaka na kuelekea nchini Chad ili kukimbia mapigano yanayoendelea pia katika mkoa wa magharibi wa Darfur.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres  ametoa wito kwa pande mbili hasimu nchini Sudan kufikia makubaliano ya usitishaji mapigano kwa muda wa siku tatu wakati wa sikukuu ya Waislamu ya Eid el-Fitr ili kuruhusu raia kufika katika maeneo salama. Guterres amesema raia wamenaswa katika maeneo yenye migogoro na wanapaswa kuruhusiwa kuondoka ili kutafuta matibabu, chakula na vifaa vingine.

Marekani ambayo imekubaliana pia na pendekezo hilo la kusitisha mapigano, imesema inatuma wanajeshi zaidi katika eneo hilo ili kujiandaa ikiwa italazimika kuwahamisha wafanyakazi wa ubalozi wake mjini Khartoum. Guterres na maafisa wakuu kutoka Marekani, Saudi Arabia, Qatar, Uturuki na Misri wamemtaka mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan kusitisha ghasia.

Soma pia: RSF: Tuko tayari kusitisha mapigano Sudan

Sudan | Kämpfe in Khartoum
Jengo lililoshambuliwa kwa makombora mjini Khartoum, Sudan (20.04.2023)Picha: Omer Erdem/AA/picture alliance

Zaidi ya watu 330 wameuawa hadi sasa katika ghasia hizo za kuwania madaraka zilizozuka mwishoni mwa jumaa iliyopita kati ya viongozi wawili tawala na washirika wa zamani wa jeshi nchini Sudan.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungungumzo kwa njia ya video na wakuu wa Umoja wa Afrika, Jumuiya ya nchi za Kiarabu na mashirika mengine, Guterres amesema kulikuwa na makubaliano madhubuti juu ya kulaani mapigano yanayoendelea nchini Sudan na kwamba kipaumbele ni kuhimiza usitishwaji wa ghasia.

Burhan na Dagalo wakubali kusitisha mapigano

Burhan amekiambia kituo cha habari cha Al Jazeera kuwa anaunga mkono makubaliano ya kusitisha mapigano kwa sharti la kuwaruhusu raia kusafiri kwa uhuru, jambo ambalo amesema, hadi sasa limekataliwa na vikosi vya RSF, na kusisitiza kuwa sasa haoni mshirika wa mazungumzo, na hana chaguo jingine ila suluhisho la kijeshi.

Soma pia: Mapigano ya Sudan yaingia siku ya sita na kuua watu 300

Kombobild Abdul Fattah Al-Burhan und Mohamed Hamdan Dagalo
Kiongozi wa vikosi vya RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo (Kulia) na mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan Picha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Mpinzani wake na kiongozi wa vikosi vya RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, ameiambia pia Al Jazeera kwamba yuko tayari kutekeleza makubaliano ya usitishwaji mapigano kwa muda wa siku tatu kwa ajili ya sikukuu ya Eid, ambayo inaashiria kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Dagalo, anayefahamika pia kama Hemedti, amesema mara kadhaa kuwa yeye anaunga mkono makubaliano ya usitishaji vita kwa muda mfupi lakini makubaliano hayo kila mara yamekuwa hayatekelezwi.

Mapigano yanayoendelea nchini Sudan kati ya majeshi yanayowatii majenerali wawili wakuu yanaiweka nchi hiyo ya tatu kwa ukubwa barani Afrika katika hatari ya kutumbukia katika mzozo mkubwa zaidi ambao unaweza kuwa matokeo mabaya si kwa nchi hiyo pekee bali kwa sehemu kubwa ya ukanda huo.