Makubaliano ya kusitisha mapigano yavunjika Sudan
19 Aprili 2023Jumatano (Aprili 19) iliamkia kwa mashambulizi mengine ya anga na miripuko katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, baada ya kushindwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani baina ya jeshi rasmi na wapiganaji wa kikosi maalum cha wanamgambo kinachoogopewa cha RSF, huku maelfu ya wakaazi wa mji huo wakijaribu kuyakimbia mapigano hayo.
Milio ya makombora na miripuko iliendelea kusikika hadi asubuhi ikitokea yalipo makao makuu ya wizara ya ulinzi na uwanja wa ndege, ambayo yamekuwa yakiwaniwa na pande hizo mbili tangu mapigano yalipoanza mwishoni mwa wiki iliyopita.
Soma zaidi: Milio ya risasi inaendelea kusikika nchini Sudan licha ya kauli ya kusitisha mapigano
Mashahidi mjini Khartoum walisema "anga zima la mji huo mkuu limejaa moshi."
Mataifa ya kigeni, ikiwemo Marekani, yamekuwa yakishinikiza makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya jeshi la vikosi vya RSF ili kuwapa nafasi raia kupata misaada na huduma muhimu.
Kila upande waushutumu mwengine
Awali pande zote mbili zilikuwa zimeashiria kukubaliana na kusitisha mapigano kutoka saa 12:00 jioni ya Jumanne (Aprili 18), lakini muda mfupi baadaye milio ya risasi na makombora ilisikika na kila upande ulitowa taarifa ya kuushutumu mwengine kwa kutoheshimu makubaliano hayo.
Kwa upande wake, kamandi kuu ya jeshi ilisema wale inaowaita "wanamgambo waasi" wameendelea na kusababisha ghasia za hapa na pale kuzunguka makao makuu ya jeshi na uwanja wa ndege", huku taarifa ya RSF ikisema jeshi "limeendelea kuyavunja makubaliano ya kusimamisha mapigano" kwa kuzishambulia kambi zake kwenye mji mkuu, Khartoum.
Soma zaidi: Sudan: Kuna kauli zinazokinzana juu ya usitishaji mapigano
Shirika la habari la Reuters linaripoti kwamba mapigano yalianza tena usiku na kisha kurejea tena alfajiri ya leo kwenye upande wa mashariki mwa mji mkuu, Khartoum, ambako wakaazi wanasema muda pekee ambao kulikuwa kimya ni baina ya saa 9:00 na 11:00 asubuhi.
Wakaazi wa Khartoum wakimbia
Shirika la habari la AFP linaripoti kuwashuhudia maelfu ya wakaazi wa mji huo wakikimbia makaazi yao, wengine kwa magari na wengine kwa miguu, wakiwamo wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa wakaazi hao, mitaa yao "imejaa miili na harufu za maiti."
Soma zaidi: Msafara wa ubalozi wa Marekani washambuliwa Sudan
Baadhi ya serikali za mataifa ya kigeni zimeanza mipango ya kuwahamisha maelfu ya raia wao, wakiwemo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.
Japan imesema hivi leo kwamba wizara yake ya ulinzi imeanza matayarisho ya kuwaondoa raia wake 60 waliopo nchini Sudan, wakiwemo wafanyakazi wa ubalozi.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, idadi ya waliokwishauawa kwenye mapigano hayo inatajwa kufikia 185 huku zaidi ya 1,800 wakijeruhiwa, ingawa Chama cha Madaktari kinaripoti kwamba idadi kamili huenda ikawa kubwa zaidi ya hapo, kwani wengi wa waliouawa na kujeruhiwa hawafikishwi hospitalini kutokana na mashambulizi.
Vyanzo: Reuters, AFP