Spain yaishinda France 2-1 kufika fainali ya EURO 2024
10 Julai 2024Kikosi cha Kocha Didier Deschamps kilitangulia mbele kupitia bado lililofungwa na Randal Kolo Muani lakini Lamine Yamal alisawazisha muda mfupi baadae na kuwa mgungaji kinda zaidi katika historia ya michuano hiyo, huku bao la Dani Olmo katika dakika ya 25 likiihakikishia ushindi Uhispania.
Uhispania ni timu ya kwanza kushinda mechi sita michuano ya Euro
Mabingwa mara tatu Uhispania wamekuwa timu ya kwanza kushinda mechi sita kwenye Michuano ya Euro na wamebakiza mchezo mmoja kushinda taji la kuvunja rekodi la nne.
Soma pia:Uhispania na Ufaransa kutunishiana misuli nusu fainali ya EURO 2024
Maswali yataulizwa namna Wafaransa, ambao wamefika fainali mara tatu katika michuano minne iliyopita, wameshindwa kutambaa mbele ya Uhispania licha ya kujivunia vipaji vikubwa vya ushambuliaji.
Ufaransa walikuwa wamefunga mabao matatu tu kuelekea mechi hiyo, na kati ya hayo hakuwa hata moja lililofungwa na mchezaji wa Ufaransa kwenye mchezo wa wazi na kocha Didier Deschamps alishughulikia hali hiyo kwa kumuweka benchi fowadi Antoine Griezmann na kumuingiza Ousmane Dembele.
Soma pia:Euro2024: Uhispania yawatoa wenyeji Ujerumani robo fainali
Yamal alitengeeza nafasi ya kwanza ya mechi hiyo dakika nne baada ya mchezo kuanza, kwa krosi ya juu iliyomfikia Fabian Ruiz, ambaye kichwa chake kilikwenda juu ya lango la Ufaransa. Dakika nne baadaye, Mbappe alimpigia krosi Kolo Muani, ambaye alifunga bao lililoipa uongozi Ufaransa.
Wakati mashaka ya kabla ya mechi yaliwalenga wakongwe wa Uhispania Jesus Navas mwenye umri wa miaka 38, na Nacho mwenye miaka 34, ambao walichukua nafasi za Dani Carvajal na Robin Le Normand, vijana Aymeric Laporte na Marc Cucurella walifanya makosa yaliochangia bao la kwanza la Kolo Muani.
Yamal ni mfungaji mdogo zaidi katika historia ya EURO
Bao la Ufaransa lilionekana kuondoa upepo kwa Uhispania lakini alikuwa mchezaji mdogo zaidi uwanjani aliefunga bao maridadi kabisaa la kusawazisha.
Bao hilo lilimfanya Yamal, ambaye tayari amesaidia mabao matatu kwenye michuano ya Euro 2024, kuwa mfungaji mdogo zaidi katika historia ya mashindano hayo, akiipiku rekodi ya awali kwa mwaka mmoja na nusu.
Soma pia:Mbappe avunjika pua katika ushindi wa Ufaransa dhidi ya Austria
Bao la Lamal, dakika 13 baada ya bao la kwanza la Ufaransa, liliamsha mashambulizi ya Uhispania na vijana hao wa La Roja walipata bao la kuongoza dakika nne baadaye kupitia kwa Olmo.
Nafasi bora zaidi kwa Ufaransa ya kulazimisha muda wa nyongeza iliangukia kwa nahodha wao zikiwa zimesalia dakika tano, lakini Mbappe alipiga shuti lake juu akiwa amebaki na kipa Unai Simon pekee.
Uhispania walikuwa bora
Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps, amekiri kuwa Uhispania walikuwa bora licha ya vijana wake kutangulia kufunga bao.
Hapo kesho England itacheza dhidi ya Uholanzi katika mechi ya pili ya nusu fainali, itakayoamua nani ataungana na Uhispania siku ya Jumapili mjini Berlin.