Euro 2024: Spain yawatoa wenyeji Germany robo fainali
6 Julai 2024Dani Olmo ndiye aliyepachika goli la kwanza la Uhispania katika dakika ya 51, ambalo lilirejeshwa na Florian Witz wa Ujerumani katika dakika ya 89, kabla ya Mikel Merino kuandika ushindi kwa mkwaju wa dakika za nyongeza.
Merino mwenye umri wa miaka 28 alishangiria kwa kuigiza staili ya baba yake, Miguel Merino. Aliwaambia waandishi wa habari kwamba goli lake ni alama ya kihistoria kwenye uwanja wa Stuttgart, ambako zaidi ya miongo mitatu iliyopita, baba yake alipachika goli la ushindi kwa timu yake ya Osasuna dhidi ya Sttutgart Novemba 1991.
Soma zaidi: Euro 2024: UEFA yaunda mfumo wa kuwasilisha malalamiko ya haki za binadamu
Kocha wa Uhispania, Luis de la Fuente, ameiita mechi hiyo kuwa mashindano ya farasi, huku akisema anajivunia kuwafundisha wachezaji walioonesha kiwango cha juu cha mchezo.
Ufaransa yaitowa Ureno
Kwa upande mwengine, mechi kati ya Ureno na Ufaransa ilimalizikia kwa mikwaju ya penalti baada ya dakika za kawaida na za nyongeza kumalizika bila timu yoyote kuliona lango la mwenzake.
Ufaransa imeiangusha Ureno kwa mikwaju mitano kwa mitatu.
Soma zaidi: Mbappe avunjika pua katika ushindi wa Ufaransa dhidi ya Austria
Mkongwe wa soka la kulipwa, Cristiano Ronaldo alitoka uwanjani bila kuipatia Ureno goli lolote lile, ikiwa ni mara ya kwanza kwenye historia yake ya soka.
Kocha wa Ufaransa, Didier Dechamps, amesema ushindi wao ulipatikana kwa tabu kwa kuwa wamecheza na mojawapo wa timu bora kwenye kandanda ya Ulaya.
Uturuki yakasirishwa na UEFA
Hayo yakijiri, serikali ya Uturuki imeghadhibishwa na kile ilichosema ni hukumu isiyo ya haki na inayoegemea upande mmoja ya kufungiwa kwa mchezaji wake, Merih Demiral, kutocheza mechi mbili, ikimaanisha kuwa ataukosa mchezo wa leo na Uholanzi.
Demiral alikuwa nyota wa mchezo kati ya nchi yake na Austria ambapo Uturuki ilishinda 2 kwa moja, na wakati wa kusherehekea goli lake la pili, alionesha ishara inayohusishwa na kundi la siasa kali za mrengo wa kulia la Uturuki, Grey Wolves.
Soma zaidi: Conceicao aipa ushindi Portugal kwa bao la dakika za mwisho
Uongozi wa UEFA unasema umemfungia Demiral kwa kosa la kuvunja kanuni za msingi za tabia njema, hatua ambayo Waziri wa Michezo wa Uturuki, Osman Askin Bak, anadai imechochewa kisiasa, huku kocha wa timu hiyo, Vincenzo Montella, akisema ni hukumu iliyotokana na kutoelewa utamaduni wa Uturuki, ambayo kwao alama ya mbwa mwitu ni kielelezo cha watu wao.
Katika mechi ya leo saa tatu usiku kwa majira ya hapa Ulaya ya Kati, timu ya Uturuki inacheza na Uholanzi mjini Berlin, ambapo Rais Tayyip Erdogan anatazamiwa kuhudhuria.
Mechi hiyo itatanguliwa na ile ya England na Uswisi itakayochezwa saa 12 jioni.