1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shughuli ya kuhesabu kura za Wakenya inaendelea

11 Agosti 2022

Matokeo ya awali kutoka uchaguzi huo wa jana nchini Kenya yanaashiria kuwa ushindani ni mkubwa kati ya William Ruto wa UDA na kigogo wa siasa Raila Odinga wa Azimio la Umoja One Kenya.

https://p.dw.com/p/4FMMD
Kenia Wahlen 2022
Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Kwa upande wake tume ya uchaguzi IEBC ina siku saba baada ya uchaguzi kabla ya kumtangaza mshindi. Maafisa wa tume ya uchaguzi IEBC wamekesha wakihesabu na kujumlisha kura kwenye vituo mbalimbali kote nchini.

Kufikia sasa maelezo ya fomu 34A kutokea vituo 43,536 kati ya vyote 46,229 yamewasilishwa kwenye mtandao wa tume ya uchaguzi.Kwa mantiki hii mfumo huo umefanikiwa kwa 94.17%. Kaunti ya Nairobi ndiyo inayoongoza kwenye mchakato wa kuwasilisha maelezo ya Fomu ya 34A.Wajir ndiyo inayosuasua ukizingatia kuwa wapiga kura wa eneo jimbo la Eldas ni baadhi ya yale 6 ambayo bado hawajakamilisha mchakato wa kwenda debeni.

Tume ya uchaguzi yawataka Wakenya kuvuta subira

Kenia | Wahlkampf - Wahlkommission IEBC - Wafula Chebukati
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati Picha: John Ochieng/Zuma/picture alliance

Hata hivyo hilo linatarajiwa kufanyika Jumatano hii. Akizindua rasmi shughuli ya kuhesabu na kujumlisha kura kwenye ukumbi wa Bomas of Kenya,mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, Wafula Chebukati aliwarai wakenya kuvuta subra. Tume ya uchaguzi imeandaa sehemu maalum kwenye mtandao wake ambako maelezo ya fomu 34A na B yatachapishwa kwa umma kuyatazama kadri yanavyobadilika.

Ifahamike kuwa wakenya wanaoishi kwenye mataifa 12 ya kigeni pia wamefanikiwa kupiga kura kumchagua rais pekee.Mataifa hayo ni yale ya jirani ambayo ni nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,Canada, Ujerumani,Marekani,Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Soma zaidi:Ruto na Odinga jino kwa jino Kenya

Kwa upande mwengine,shule za msingi zitafunguliwa Jumatatu ijayo ya tarehe 15 Agosti badala ya kesho kama ilivyotangazwa awali.Waziri wa elimu Profesa George Magoha alitangaza hilo baada ya mashauriano ukizingatia kuwa baadhi ya shule zinatumiwa kuhesabia na kujumlisha kura.Gazeti rasmi la serikali linabainisha kuwa shule 250 za msingi na sekondari zinatumika kama vituo vya kuhesabia kura.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya/DW Nairobi

Mhariri: Daniel Gakuba