Shambulio la Israel kwenye shule ya Gaza lalaaniwa kimataifa
10 Agosti 2024Francesca Albanese, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya haki za binadamu katika maeneo ya Palestina amesema Israel inawaua Wapalestina kitongoji kimoja baada ya kingine, kwenye hospitali, shule, kambi za wakimbizi na hata kwenye maeneo yanayotajwa kuwa "salama".
Katika mtandao wake wa X (zamani Twitter), Albanese amesema Israel imekuwa ikifanya mashambulizi hayo dhidi ya Wapalestina kwa kutumia silaha ilizopewa na Marekani na Ulaya huku akiomba Wapalestina wawasamehe kwa kushindwa kwao kwa pamoja kuwalinda.
Soma pia: Baraza la Haki la UN lataka Israel kuwajibishwa kwa uhalifu wa kivita huko Gaza
Katika ripoti iliyotolewa mwezi Machi, Albanese alisema kulikuwa na "taarifa za kuridhisha" ya kwamba Israel ilifanya vitendo kadhaa vya "mauaji ya halaiki" katika vita vyake huko Gaza. Israel, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikimkosoa Albanese na mamlaka yake, iliishutumu ripoti hiyo na kusema "inaugeuza ukweli".
Albanese amesisitiza kwamba bila shaka alilaani pia mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas dhidi ya Israel ambayo yalianzisha vita vya miezi 11 katika Ukanda wa Gaza. Wajumbe maalum huteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lakini huwa hawazungumzi kwa niaba ya Umoja wa Mataifa.
Umoja wa Ulaya, Misri na Qatar zalaani shambulio hilo
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell siku ya Jumamosi alielezea kusikitishwa kwake na shambulizi hilo baya la Israel dhidi ya shule inayohifadhi watu waliokimbia makazi yao huko Gaza.
Borrell aliandika kwenye mtandao wa X: "Nimeshtushwa na picha za shule hiyo huko Gaza iliyokumbwa na shambulizi la Israel, na inasemekana kuwa makumi ya wahanga wa Kipalestina wameuawa. Angalau shule 10 zililengwa katika wiki zilizopita. Hakuna uhalali wa mauaji haya."
Soma pia: UN yaishtumu Israel kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, Hamas kwa uhalifu wa kivita
Wizara ya mambo ya nje ya Misri ililaani shambulizi hilo na kusema mauaji ya raia wa Gaza yanaonyesha kuwa Israel haikuwa na nia ya kusitisha vita. Wizara ya mambo ya nje imesema tukio hilo inadhihirisha ni kwa namna gani sheria za kimataifa zinapuuzwa na kwamba shambulio hilo lilikuwa ni "mwendelezo wa uhalifu wa kiwango kikubwa" dhidi ya "idadi kubwa ya raia wasio na silaha" .
Watu zaidi ya 100 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia shambulizi la Israel katika shule moja iliyokuwa ikiwahifadhi wakimbizi wa ndani katika Ukanda wa Gaza. Hayo yameelezwa Jumamosi na utawala wa Hamas unaoongoza eneo hilo. Jeshi la Israel lilidai kuwa lililenga kituo cha kamandi cha wanamgambo hao wa Kipalestina.
Mazungumzo yausitishwaji vita yatarajiwa kuanza tena
Misri, Marekani na Qatar wamepanga duru mpya ya mazungumzo ya kusitisha mapigano siku Alhamisi, wakati hofu ikiongezeka ya kutokea mzozo mkubwa zaidi wa kikanda, utakaozihusisha Iran na Lebanon.
Saudi Arabia imepongeza hatua ya mataifa hayo matatu wapatanishi ya kuzialika Israel na Hamas kurejea kwenye mazungumzo ya kusitisha mapigano ambayo yanatarajiwa kufanyika Agosti. 15, na kuthibitisha msaada wake kamili kwa jopo hilo ili kushughulikia kwa haraka kuzorota kwa hali ya kibinadamu huko Gaza.
Uturuki kwa upande wake imesema shambulio hilo dhidi ya shule huko Gaza ni 'uhalifu mpya dhidi ya ubinadamu' uliofanywa na Israel na kusababisha vifo vya raia zaidi ya 100 waliokuwa wamekimbilia kwenye shule hiyo. Serikali ya Ankara imemtuhumu pia Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa kuhujumu mchakato wa mazungumzo ya usitishwaji mapigano Gaza.
Wakati vita vikiendelea katika Ukanda wa Gaza, wizara ya Afya eneo hilo inayodhibitiwa na Hamas imesema hadi sasa idadi ya vifo imefikia watu 39,790.
Hofu ya kuzuka kwa vita vya kikanda Mashariki ya Kati
Kiongozi mkuu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq Ayatollah Ali Sistani ameonya Jumamosi juu ya hatari ya kuongezeka kwa uwezekano wa kutokea vita vya kikanda vitakavyokuwa na "matokeo mabaya" kufuatia mauaji ya viongozi wawili wa wanamgambo Hamas na Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran.
Sistani pia amehimiza kukomeshwa kwa "vita vya mauaji ya halaiki" huko Gaza. Eneo la Kanda ya Mashariki ya Kati liko katika hali ya tahadhari baada ya Iran kuapa kuwa italipiza kisasi mauaji ya Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh mjini Tehran huku kundi la Hezbollah likitoa kauli kama hiyo kufuatia mauji ya kamanda wake Fuad Shukur mjini Beirut.
Mataifa mbalimbali yamekuwa yakijaribu kutumia mikakati ya kidiplomasia ili kupunguza hali ya mivutano kati ya Israel na Iran na hivyo kuepuka vita vya kikanda ambavyo bila shaka vitakuwa na athari kubwa.
(Vyanzo: AP, DPAE, Reuters, AFP)