Israel yakabiliwa na shinikizo kubwa kuhusu vita vyake Gaza
5 Aprili 2024Shirika la misaada lenye makao yake makuu nchini Marekani la World Central Kitchen - WCK ambalo wafanyakazi wake waliuawa katika shambulio la droni Jumatatu usiku, limesema litaunda tume huru ya kuchunguza mauaji hayo. Poland imedai kufanyike uchunguzi wa jinai kwa kile ilichokiita "mauaji" ya wafanyakazi wa misaada.
Israel imekiri kufanya makosa lakini ikajitetea kuwa katika shambulio hilo, ilikuwa ikimlenga mshambuliaji wa kundi la Hamas. Serikali mjini Tel-Aviv imetangaza kuwafuta kazi maafisa wawili wa jeshi na kwamba itawachukulia wengine kadhaa hatua za kinidhamu kufuatia tukio hilo ambalo awali Israel ilisema ni la kusikitisha na ambalo halikukusudiwa.,
Soma pia: Marekani, Uingereza na EU zalaani mauaji kwa watoa misaada
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema ni muhimu kuona Israel inawajibika kikamilifu kwa tukio hili na pia kuchukua hatua za kuwawajibisha wale wote waliohusika.
Israel kuruhusu misaada zaidi kuwasilishwa Gaza
Israel imetangaza mapema leo kuwa itaruhusu "kwa muda" uwasilishaji wa misaada katika eneo lililo hatarini kukumbwa na janga la njaa huko kaskazini mwa Gaza, saa chache baada ya Marekani kuonya uwezekano wa kuchukua hatua zenye mabadiliko makubwa katika sera yake kuhusu vita vya Israel dhidi ya kundi la Hamas.
Ujerumani kwa upande wake imesema Israel haina "visingizio zaidi" vya kuchelewesha hatua za kuwasilisha misaada, baada ya karibu miezi sita ya vita.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hatua mbalimbali zinazochukuliwa ili kuwezesha misaada kuwasili Gaza hazitoshi hata kidogo huku akisema kuwa anatumai kwa dhati kuwa Israel itazidisha ufanisi katika suala hilo kwa kuwa hali huko Gaza ni ya kukatisha tamaa.
Aidha Guterres ameendelea kwa kuelezea wasiwasi wake mkubwa kufuatia ripoti inayosema kwamba Israel imekuwa ikitumia teknolojia ya akili bandia ili kubaini maeneo ya kushambuliwa huko Gaza:
"Pia nimesikitishwa sana na ripoti kwamba operesheni ya jeshi la Israel ya kufyetua mabomu inajumuisha teknolojia ya akili bandia ambayo inatumiwa kama chombo cha kuwatambua walengwa wa mashambulizi hayo, hasa katika maeneo yenye wakazi wengi, na kusababisha kiwango kikubwa cha vifo vya raia. Maamuzi yanahusu maisha au kifo na ambayo huweza kuathiri familia nzima, hayapaswi kuchukuliwa kwa kuzingatia aina hii ya mahesabu."
Soma pia: Baraza la Haki la UN lataka Israel kuwajibishwa kwa uhalifu wa kivita huko Gaza
Vita hivi vilivyodumu kwa miezi sita na ambavyo vimesababisha vifo vya Wapalestina zaidi ya 33,000 vimeiweka Israel chini ya shinikizo kubwa la kimataifa ambalo limeongezeka leo baada ya Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio linalotaka Israel iwajibishwe kwa uhalifu wa kivita na ukiukwaji mwingine wa sheria za kimataifa, lakini pia kuyataka mataifa mbalimbali kusitisha uuzaji wa silaha na vifaa vya kijeshi kwa taifa hilo.
(Vyanzo: Mashirika)