Scholz: Ujerumani kupiga marufuku shughuli za Hamas
12 Oktoba 2023Scholz amesema pia katika hotuba yake mbele ya bunge siku ya Alhamisi kwamba mtandao wa mshikamano na Palestina ujulikanao kama Samidoun utapigwa marufuku.
Hamas tayari inaorodheshwa kama kundi la kigaidi na Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya, ambao Ujerumani ni mwanachama wake.
Kauli ya Scholz kuhusu Jumuiya ya Samidoun, inatokana na hatua ya wafuwasi wake kuonekana wakishangilia kwa kugawa peremende katika wilaya ya Neukölln ya Berlin, baada ya Israel kushambuliwa Jumamosi iliyopita.
Scholz: Ujerumani kama taifa halikubaliani na vitendo vya chuki dhidi ya Wayahudi.
Akizungumza kwa msisitizo kansela huyo wa Ujerumani ametaka kitendo hicho kipuuzwe, akisema sio cha kiutu na kinapingana na maadili yote ya kitaifa. Amesema Ujerumani kama taifa hawakubaliani na vitendo vya chuki, uchochezi wala chuki dhidi ya Wayahudi.
Ajenda ya mahusiano kati ya Israel na mataifa ya kiarabu
Aidha amesema kwa ujumla shambulizi la Hamas litakuwa na athari kubwa katika mahusiano ya Ujerumani na Palestina akisema misaada yote ya kimaendeleo kwa mamlaka Palestina itatathiminiwa upya. Kigezo chao katika hilo kitakuwa kuhoji kama miradi ya Ujerumani katika eneo hilo inasaidia katika ustawi wa amani na kusaidia katika usalama wa Israel.
Blinken awasili Israel huku vita vya Gaza vikiendelea
Scholz pia alimkosoa Mahmoud Abbas, kiongozi wa Mamlaka ya Palestina ambayo inasimamia kwa sehemu fulani Ukingo wa Magharibi, na viongozi wengine Palestina kwa kutolaani kwa uwazi mauaji hayo yaliofanywa na Hamas dhidi ya Waisraeli, akisema "Kimya chao ni cha fedheha,"
Ujerumani kuisaidia Israel
Aidha pamoja na kutoa ahadi ya kuisaidia kijeshi Israel dhidi ya Hamas, Kansela Scholz, amegusia tuhuma za kuhusishwa Iran, kutoa msaada wake kwa Hamas katika shambulizi hilo la Jumamosi.
Upinzani nchini Israel waungana kukabiliana na Hamas
"Hadi wakati huu, hatuna ushahidi wa kina kwamba Iran imetoa usaidizi madhubuti na wa kiutendaji kwa shambulio hili la woga la Hamas. Lakini ni wazi kwetu sote kwamba bila uungwaji mkono wa Iran katika miaka michache iliyopita, Hamas isingeweza kufanya shambulizi hilo lisilo na kifani katika ardhi ya Israel," amesema Scholz.
Katika hutuba yake hiyo ya bungeni leo pia ameonya kuwa kwa mazingira yalivyo katika Ukanda wa Gaza, mateso na ugumu wa maisha kwa raia vitaongezeka.
Israel yaendeleza mashambulizi Gaza
Israel inafanya mashambulizi mfululizo dhidi ya eneo hilo la pwani la Wapalestina na lenye idadi kubwa ya watu huku ikizuwia uingizaji wa chakula, mafuta na dawa, na kusababisha onyo kali kuhusu hali mbaya inayowakabili raia wa Gaza.
Hamas, kundi la wanamgambo linalotawala Gaza, lilifanya shambulizi kubwa la kushtukiza dhidi ya jamii za raia wa Israeli siku ya Jumamosi. Israel ilijibu kwa mashambulizi ya anga yanayoendelea dhidi ya eneo hilo ambapo zaidi ya watu 1,200 wameripotiwa kuuwawa kutoka kila upande.
Chanzo; DPA