Mashambulizi Israel, Gaza yaingia siku ya sita
12 Oktoba 2023Netanyahu alitangaza siku ya Jumatano (Oktoba 11) makubaliano ya kuunda baraza maalum la mawaziri linalowahusisha wajumbe kutoka upinzani kwa ajili ya wakati huu wa vita vyake kwenye Ukanda wa Gaza.
Kutokea Gaza nako, wanamgambo wa Hamas waliripotiwa kuendelea kurusha makombora kuelekea Israel.
Mbali na mashambulizi kutoka angani, wakaazi wa Gaza wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinaadamu, baada ya kinu pekee cha umeme kwenye ukanda huo kuishiwa na mafuta na kufungwa siku ya Jumatano.
Soma zaidi: Mzozo kati ya Israel na Hamas wazidi kutokota
Hospitali zilizolemewa zimeanza kulazimika kutumia majenereta kutoa huduma kwa idadi kubwa ya majeruhi wanaoitibiwa huko.
Hii ni kufuatia hatua ya Israel kuanzisha mzingiro kamili dhidi ya Gaza siku ya Jumatatu, ambapo waziri wake wa ulinzi alitangaza kuzuwia chakula, mafuta na huduma zozote kuufikia ukanda huo ambao tangu hapo ulishakuwa kwenye mzingiro kwa muda mrefu.
Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binaadamu yaliutaja uamuzi huo kuwa ni sawa na uhalifu wa kivita.
Idadi ya watu waliokwishauawa pande zote mbili za mzozo huu sasa imepindukia 2,300.
Juhudi za kimataifa kusitisha mapigano
Kwa upande wa jitihada za kimataifa kusitisha mashambulizi yanayoendelea sasa, Marekani ilisema hapo jana kwamba inashirikiana na Israel na Misri ili kufungua njia salama kwa raia walioko Gaza kuondoka kwenye ukanda huo.
Rais Joe Biden wa Marekani alizungumza kwa mara ya nne na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizidi kumuhakikishia uungaji mkono usio na shaka wa Washigton kwa Tel Aviv, na akiendelea kulilaani kundi la Hamas, alilosema mashambulizi yake ya siku ya Jumamosi kwa Israel yalikuwa mabaya zaidi kwa Wayahudi tangu yale mauaji ya maangamizi yaliyofanyika Ulaya dhidi ya jamii hiyo, maarufu kama Holocaust.
Hamas inazingatiwa na Marekani, Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani na baadhi ya mataifa mengine kuwa kundi la kigaidi.
Hata hivyo, Biden alisema kuwa alimuambia Netanyahu kuwa ni lazima kwa Israel kufuata kanuni za kivita wakati huu ikilipiza kisasi chake dhidi ya Hamas.
Uturuki nayo, ambayo hailichukulii kundi la Hamas kuwa la kigaidi, inaendelea na juhudi za kuachiwa kwa raia waliotekwa na wanamgambo hao, kwa mujibu wa afisa mmoja wa serikali ya Ankara, ambaye alikataa kutajwa jina lake.
Rais Ibrahim Rais wa Iran amezungumza na Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, kwa mara ya kwanza kujadiliana juu ya mgogoro huo, kwa mujibu wa shirika la habari la Iran (IRNA).
Kwa mujibu wa shirika la habari la Saudia, SPA, Bin Salman alimuambia Raisi kwamba Riyadh inaendelea kuwasiliana na wahusika wa kimataifa na kikanda kujaribu kusimamisha mapigano ya sasa kwenye Ukanda wa Gaza, ambako Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu 338,000 wamekimbia makaazi yao.
Vyanzo: AP, Reuters