Saudia Arabia yaonya juu ya vita vya Gaza kudhoofisha uchumi
28 Aprili 2024Saudi Arabia imehimiza juu ya utulivu wa kikanda na kuonya juu ya athari za vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza jinsi vinavyodumaza uchumi wa dunia, wakati mkutano wa kilele wa Jukwaa la Kimataifa la Uchumi Duniani WEF, ukifunguliwa mjini Riyadh.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, viongozi wa Palestina na maafisa wengine wa ngazi ya juu kutoka nchi tofauti, wanaojaribu kutafuta makubaliano ya usitishaji mapigano baina ya Israel na kundi la Hamas, ni miongoni mwa washiriki wa mkutano huo.
Waziri wa fedha wa Saudia Mohammed al-Jadaan alisema katika mojawapo ya mijadala ya kwanza ya mkutano wa kilele wa siku mbili kuwa vita vya Gaza, mgogoro wa Ukraine na mingineyo, vimetoa shinikizo kubwa katika uchumi wa dunia.
Rais wa Jukwaa la Kimataifa la Uchumi Duniani WEF Borge Brende, aliwaeleza waandishi wa habari siku ya jumamosi kwamba kumekuwa na msukumo mpya katika mazungumzo ya kuwaachia mateka ambao bado wanashikiliwa na Hamas, na uwezekano pia wa kutatua mzozo wa Gaza.