Ruto na Museveni wahimiza ushirikiano barani Afrika
3 Januari 2025Ruto na Museveni wameyasema hayo kwenye maadhimisho ya sherehe za jamii ya Waluo zilizowaleta pamoja Waluo kutoka Kenya, Uganda, Tanzania, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, jimboni Siaya, Nyanza nchini Kenya.
Wakimpigia debe Raila Odinga anayewania nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Museveni amesema taifa la Uganda linaunga mkono azma ya Odinga na kusistiza kuwa, ushindi wake utaleta manufaa makubwa ikizingatiwa uhusiano mzuri na tajriba aliyo nayo Odinga katika kushawishi wawekezaji na maendeleo.
Soma pia: Hasira zaongezeka Kenya kuhusiana na utekaji wa wakosoaji
Rais Ruto amesema alifanya mazungumzo na Rais Museveni kabla ya kumuidhinisha Odinga kuwania wadhifa huo, akisema kugombea kwake kupo imara zaidi kutokana na kuwashirikishwa viongozi kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
Kulingana na Ruto, Odinga yupo katika nafasi bora ya kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili Afrika ikiwemo vita katika baadhi ya mataifa, kando na uimarishaji mifumo ya kibiashara na utangamano inayohimiza utekelezwaji wa biashara huria.