1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rubiales atafikishwa mahakamani Ijumaa

12 Septemba 2023

Aliyekuwa rais wa Shirikisho la soka la Uhispania Luis Rubiales atatoa ushahidi mbele ya Mahakama Kuu mjini Madrid siku ya Ijumaa kuhusu madai yake ya kumbusu mdomoni Jenni Hermoso.

https://p.dw.com/p/4WFuN
Fußball Spanien RFEF Präsident Luis Rubiales
Picha: RFEF/AFP

Tukio hilo, lililotokea wakati wa hafla ya kutuzwa medali kufuatia ushindi wa timu ya wanawake ya Uhispania katika Kombe la Dunia huko Sydney, Australia, mwezi uliopita, liliibua wimbi la hasira dhidi ya ubaguzi wa kijinsia na tabia ya mfumo dume nchini Uhispania.

Soma pia: Rais wa Shirikisho la Kandanda la Uhispania Luis Rubiales ajiuzulu

Awali Rubiales alikataa shinikizo la kujiuzulu kutoka kwa wachezaji wengi, mashirika ya michezo na wanasiasa kutoka kwa wadhifa wake kama rais wa Shirikisho la Soka la Uhispania, akisema hajafanya chochote kibaya na busu hilo lilikuwa la hiari na makubaliano.

Hata hivyo, hasira haikuisha na Jumapili alijiuzulu baada ya Hermoso kuwasilisha malalamiko ya kesi ya uhalifu dhidi yake. Atafikishwa mbele ya mahakama saa sita mchana siku ya Ijumaa.

Soma pia: Jorge Vilda afutwa kazi kama kocha wa timu ya wanawake ya Uhispania

Je, busu lilikuwa la ridhaa?

FIFA Fußball Frauen-WM | Luis Rubiales küsst Jennifer Hermoso
Picha: Noe Llamas/Sport Press Photo/ZUMA Press/picture alliance

Malalamiko ya Hermoso yanaeleza jinsi Rubiales alivyombusu mdomoni "bila ridhaa yake" huku akishika kichwa chake kwa mikono miwili baada ya Uhispania kuishinda Uingereza katika fainali ya Kombe la Dunia la wanawake Agosti 20. Tukio hilo lilifanyika mbele ya hadhira ya televisheni ya kimataifa.

Jaji wa Mahakama Kuu Francisco de Jorge ndiye anayesimamia uchunguzi kwasababu kisa hicho kilifanyika nje ya Uhispania.

Rubiales hajajibu maswali yoyote kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu kesi hiyo.