1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jorge Vilda afutwa kazi kama kocha wa Uhispania

5 Septemba 2023

Shirikisho la soka la Uhispania RFEF limemfuta kazi kocha wa timu ya taifa ya wanawake iliyoshinda Kombe la Dunia Jorge Vilda, kufuatia sakata la Luis Rubiales kumpiga busu mdomoni Jenni Hermoso.

https://p.dw.com/p/4Vz46
Kocha wa timu ya taifa ya wanawake ya Uhispania Jorge Vilda
Kocha wa timu ya taifa ya wanawake ya Uhispania Jorge VildaPicha: Carl Recine/REUTERS


Bodi mpya iliyoundwa baada ya kusimamishwa kazi kwa Rais wa shirikisho hilo Luis Rubiales imeamua kwa sauti moja kusitisha mkataba wa Vilda, anayechukuliwa kuwa mshirika wa karibu wa Rubiales.

Shirikisho hilo pia “limeomba radhi” kwa kile ilichokiita tabia isiyokubalika ya Rubiales.


Rubiales mwenye umri wa miaka 46, aliibua ukosoaji mkubwa duniani baada ya kumbusu kwa lazima mchezaji wa timu ya taifa ya Uhispania Jenni Hermoso wakati wa hafla ya kutoa medali kufuatia ushindi wa Uhispania dhidi ya timu ya taifa ya Uingereza mnamo Agosti 20.


Rais huyo wa RFEF tayari amesimamishwa kazi na FIFA ili kupisha uchunguzi japo amekataa kabisa kujiuzulu, na kujitetea kuwa busu lake na Hermoso lilikuwa tukio la kukubaliana.


Hermoso hata hivyo amekanusha madai ya Rubiales na kuongeza kuwa, alihisi kama "mhanga wa unyanyasaji."