1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Nigeria yalaumiwa kwa kusababisha vifo

17 Desemba 2018

Shirika la kutetea haki za binadamu limesema serikali ya Nigeria imesababisha vifo vya watu zaidi ya 3500 kutokana na kushindwa kuchukua hatua ili kuzuia mapigano kati ya wakulima na wafugaji.

https://p.dw.com/p/3AGEi
Niger Kämpfer
Picha: picture-alliance/dpa

Shirika la Amnesty International limebainisha kwamba aslimia 57 ya vifo 3,641 vimetokea mnamo mwaka  huu. Asasi hiyo imesema mauaji hayo yametokea licha ya majeshi ya usalama kuwekwa karibu na sehemu ambako mapigano yalitokea. Shirika hilo limesema katika ripoti yake kwamba mara kadhaa majeshi ya usalama yalikuwa karibu na sehemu ambako mapigano yalitokea lakini yalichelewa kuchukua hatua. 

Kwa jumla watu 3641 waliuawa mnamo kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Asasi hiyo imesema hali hiyo imetokea kutokana na serikali kushindwa kuchunguza na kuwachukulia hatua waliosababisha ghasia hizo.

Mkurugenzi wa shirika la Amnesty International nchini Nigeria Osai Ojigho ameeleza kwamba

serikali ya Nigeria imeonyesha kiwango kikubwa cha uzembe, na imeshindwa kulitekeleza jukumu lake la kuyalinda maisha ya wananchi na kuukomesha mgogoro mkubwa kati ya wakulima na wafugaji. Amesema uzembe wa serikali umetoa mwanya wa kuendelea kwa mauaji, bila ya wahalifu kuchukuliwa hatua.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu la Amnesty international lilianza kuorodhesha mapigano kati ya wakulima na wafugaji kuanzia mwezi Januari mwaka 2016. Uchunguzi ulifanyika kwenye vijiji 56 katika majimbo matano ya Nigeria.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari
Rais wa Nigeria Muhammadu BuhariPicha: picture-alliance/empics

Kwa mujibu wa taarifa ya Amnesty International majeshi ya usalama mara nyingine yalipewa taarifa za tahadhari mapema, juu ya uwezekano wa kutokea mapigano kati ya wakulima na wafugaji lakini hakuna hatua za haraka hazikuchukuliwa kuzuia  mauaji. Kutokana na ghasia hizo, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita maalfu ya watu wameyakimbia makaazi  yao.

Shirika la Amnesty International limesema utafiti wake umeonyesha kwamba mashambulio hayo yalipangwa na kuongozwa vizuri, na kwamba silaha kama vile bunduki aina ya AK 47 zilitumika. Mkurugenzi wa asasi hiyo nchini Nigeria Osai Ojigho amesema mgogoro huo hautokani na taofauti za kidini au za kikabila.

Ameeleza kuwa wakulima na wafugaji wanapigania ardhi, kwa ajili ya kilimo na malisho lakini amesema baadhi ya wanasiasa wanajaribu kuutumia mgogoro huo kwa sababu za kisiasa. Mkurugenzi huyo ameitaka  serikali ya Nigeria ifanye uchunguzi na ichapishe matokeo yake na watakaopatikana na hatia wachukuliwe hatua za kisheria kwa njia ya haki.

Shirika la Amnesty International limesema limeipa serikali ya Nigeria matokeo ya uchunguzi wake na imeitaka wizara ya Sheria, Jeshi la Nigeria, Jeshi la Polisi na serikali za majimbo ya Adamawa, Benue, Enugu, Kaduna, Plateau na Taraba yatoe maelezo. Ni serikali ya jimbo la Enugu tu iliyotoa maelezo kwamba watu watano wanaoshutumiwa juu ya mauaji ya watu 12 wa jamii ya Nimbo wamefunguliwa mashtaka. watu hao walishambuliwa katika mtaa wa Uzo-Uwani, mnamo tarehe 25 mwezi Aprili mwaka 2016.

Mwandishi:Zainab Aziz/https://www.amnesty.org/en/latest/news/2018/12

Mhariri: Iddi Ssessanga