Rais Xi ameahidi msaada wa dola bilioni 50 kwa Afrika
5 Septemba 2024Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya China, zaidi ya viongozi 50 wa Afrika na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wanahudhuria kongamano hilo la juma hili kati ya China na Afrika.
Akihutubia viongozi hao katika hafla ya ufunguzi wa kongamano hilo katika jumba mashuhuri na la kifahari huko Beijing Xi alisifu uhusiano na bara la Afrika na China kuwa upo katika "kipindi chao bora zaidi katika historia".
Rais Xi Jinping China yaonesha utayari zaidi kushirikiana na Afrika
Amesema China iko tayari kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika katika sekta ya viwanda, kilimo, miundombinu, biashara na uwekezaji. "Katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, serikali itakuwa tayari kutoa msaada wa kifedha unaofikia dola bilioni 50.7.
Zaidi ya nusu ya kiasi hicho kitakuwa cha mkopo, na kiasi kingine cha dola bilioni 11, kitatolewa katika namna tofauti za usaidizi kikiwemo cha dola bilioni 10 kwa mpango wa kuchochea makampuni ya Kichina katika uwekezaji wake."
Kiongozi huyo wa jamhuri ya watu wa China, kadhalika ameahidi kusaidia katika uundwaji wa nafasi za kazi takribani milioni moja kwa Afrika. Ahadi nyingine imehusisha msaada wa dola milioni 141 kwa ajili ya kusaidia operesheni za kijeshi barani Afrika. Serikali ya Beijing itatoa mafunzo kwa wanajeshi 6,000 na polisi 1,000 na maafisa wa usimamizi wa sheria kutoka Afrika.
Guterres ahimiza matumizi ya nishati mbadala Afrika
Akihutubia pia mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Guterres amewaambia viongozi wa Afrika kwamba kuongezeka kwa uhusiano kati ya China na bara hilo kunaweza "kuchochea mapinduzi ya nishati mbadala." China ina rekodi ya kutolewa mifano ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kutokomeza umaskini na utaalamu katika fani na stadi mbalimbali.
Lakini mikutano ya China na taifa moja moja la Afrika iliyofanyika kando ya mkutano huo ilitoa ahadi nyingi za ushirikiano zaidi katika miradi kuanzia kwa reli, uzalishaji wa nishati ya jua biashara ya maparachichi.
Kufuatia mikutano hiyo ya Jumatano, Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amesema kuwa amesimamia makubaliano kati ya kampuni ya umeme ya nchi hiyo ZESCO na PowerChina ya Beijing ya kupanua matumizi ya nishati ya jua nchini mwake. Nigeria miundombinu, vikiwemo usafirishaji, bandari na ukanda uhuru wa kibiashara wakati Tanzania kupitia Rais Samia Suluhu Hassan amepata ahadi ya ufufuaji wa reli inayounganisha taifa lake na Zambia TAZARA.
Soma zaidi:India, China na Brazil zaweza kuwa wapatanishi, asema Putin
China, taifa lenye kuwekwa nafasi ya pili kwa nguvu za kiuchumi duniani ni mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara na Afrika na limekuwa katika juhudi za kutumia rasilimali nyingi za bara hilo ikiwa ni pamoja na shaba, dhahabu, lithiamu na madini mengine adimu.
Chanzo: AFP