Kenya yapunguza bajeti kwa shilingi bilioni 177
5 Julai 2024Kwenye mabadiliko hayo aidha, nusu ya washauri wa serikali watasimamishwa kazi. Haya yamejiri baada ya maandamano ya wiki tatu ya kuishinikiza serikali kufanya mageuzi.
Akilihutubia taifa Ijumaa alasiri, Rais William Ruto alitangaza mabadiliko makubwa serikalini yanayoashiria kulegeza msimamo kufuatia shinikizo za maandamano ya kuipinga serikali. Rais Ruto alisema atawasilisha kwenye bunge la taifa, bajeti iliyopunguzwa kwa shilingi bilioni 177 za Kenya.
Hata hivyo kiwango kilichosalia kitatoka kwenye mkopo wa kufidia pengo hilo. Hali hiyo itaiongeza nakisi ya bajeti kutokea asilimia 3.3 hadi 4.6, fedha zitakazotumika kufadhili huduma za msingi za serikali.
Ifahamike kuwa serikali ya Kenya ilihitaji shilingi bilioni 346 za ziada kufadhili mahitaji ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2024, kiwango kilichozua hisia mseto na kusababisha maandamano.
Maandamano hayo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 40 ijapokuwa serikali inaelezea idadi tofauti. Mmoja ya waliouawa ni Rex Masai aliyepigwa risasi na maafisa wa usalama kwenye maandamano wiki iliyopita na kuzikwa siku ya Ijumaa katika kaunti ya Machakos.
Soma pia:Mashirika ya haki yamesema Wakenya wengi walitekwa wiki mbili zilizopita
Kadhalika hoja ya kuwaajiri waratibu wa wizara imesitishwa pamoja na washauri wa serikali kupunguzwa kwa nusu. Wakati wa maandamano hayo, baadhi walikamatwa na kuzuiliwa na polisi na mpaka sasa hawajulikani waliko.
Alfred Keter ni mbunge wa zamani wa Nandi Hills ambaye pia alikamatwa na polisi katika mazingira ya kutatanisha aliachiliwa na siku ya Ijumaa alimkosoa vikali Rais William Ruto.
Soma pia: Ruto: "Sina hatia" na vifo vya waandamanaji
Wakenya wamekuwa wakilalamikia matumizi yaliyoongezeka ya serikali mfano kutenga afisi ya mke wa rais na naibu wake.Kutokea leo afisi hizo zimeondolewa bajeti ikiwemo pia ya waziri kiongozi.
Rais William Rutto aidha, ameteua jopo maalum la kuhakiki deni la umma na njia mujarabu za uratibu. Jopo hilo limepewa muda wa miezi mitatu kufanya kazi yake.