Rais wa zamani wa Kenya, Mwai Kibaki azikwa
30 Aprili 2022Mwili wake ulisafirishwa kwa gari kutokea Nairobi hadi Nyeri ili Wakenya wapate fursa ya kumuaga kwa mara ya mwisho na kisha maziko ya familia kufanyika.
Akiongoza ibada ya mazishi Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Nyeri, Anthony Muheria, aliwakumbusha Wakenya kuwa Rais Kibaki hakuwahi kumsema yeyote vibaya wakati wowote. Askofu Muheria aliwasihi Wakenya pamoja na waliofika kwenye ibada hiyo kuwa na imani na wepesi wa kusamehe kama alivyokuwa Kibaki.
Alisema kuwa Kibaki angewataka viongozi kusita kutoa kauli za uchochezi na badala yake kuhubiri amani. ''Tuwe wakweli na wa kusema yaliyo halisi bila ya kuwa jeuri. Tudumishe imani. Hii ina maana pia kuwa wanyenyekevu kwani hicho ni kitu kimoja cha kumuenzi alivyokuwa baba yetu Kibaki. Siku ya leo ni mfano wa jinsi alivyopenda kuishi bila makuu, kwani alitaka afanyiwe maziko ya kawaida,'' alisisitiza Askofu Muheria.
Kwenye ibada ya Jumamosi, mtoto wa kiume wa Kibaki, Jimmy Kibaki alimsifu baba yake akisema kwamba alikuwa baba ambaye aliyapa uzito masuala ya elimu. Kibaki ameacha watoto wanne na wajukuu kadhaa. Watoto wote walimminia sifa baba yao na kumtaja kuwa mzazi mzuri aliyesisitizia umuhimu wa maadili katika maisha na jamii.
Siku ya Ijumaa katika Ibada ya kitaifa David Kagai alimsifu baba yake kwa kuwa si tu baba na mzazi mzuri, bali pia mwandani wake.
Hotuba za viongozi
Rais Uhuru Kenyatta alimsifu mtangulizi wake na aliweka bayana kuwa Kibaki alikuwa baba aliyeheshimiwa na wote nchini Kenya kutokana na busara zake. Rais Kenyatta aliwahi kufanya kazi pamoja na Kibaki alipokuwa kwenye awamu ya pili ya uongozi mwaka 2008.
Kwa upande wake Naibu wa Rais, William Ruto aliukumbusha umma kuhusu mchango wa Kibaki kwenye harakati za kuwa na muundo madhubuti wa kiuchumi.
Alifafanua kuwa Kibaki alilipa uzito suala la kuwawezesha watu wa chini kutimiza malengo yao ya kiuchumi. ''Mwai Kibaki ndiye muasisi wa Kenya mpya ya kisasa. Kutokea asili yake ya kijiji cha Kanyange, alifanikiwa kujijengea jina kitaifa. Huo ndio mfano mzuri zaidi wa muundo huo wa kiuchumi,'' alifafanua Ruto.
Viongozi wa serikali walikuwako kutoa heshima zao za mwisho mjini Nyeri. Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Rais wa Afrika Kusini na mwenzake wa Ethiopia walikuwako kwenye ibada siku ya Ijumaa alipoagwa rasmi kitaifa jijini Nairobi. Shughuli hiyo iliongozwa na wanajeshi wa Kenya, KDF waliousafirisha mwili wa Kibaki kutokea Nairobi hadi Othaya.
Mizinga 19
Wakati maiti ya Kibaki ikiteremshwa kaburini mizinga 19 ilifyatuliwa kama heshima kwake. Kibaki alizaliwa mwaka 1931 na alikuwa serikalini kwa miongo mingi kama waziri, mbunge na hatimaye rais wa Kenya.
Hii ni kwa sababu alikuwa tayari amestaafu kwa muda mrefu, mizinga sawa na iliyopigwa wakati wa maziko ya mtangulizi wake marehemu Daniel Arap Moi. Ifahamike kuwa nyimbo ya taifa ya Kenya ilichezwa na bendi ya jeshi pamoja na ile ya Afrika Mashariki kwani ndiye mwenyekiti wa jumuiya hiyo.
Hii ni mara ya tatu maziko ya kitaifa ya heshima zote za kijeshi yamefanyika Kenya. Wa kwanza kupewa heshima hizo ni muasisi wa taifa hilo Jomo Kenyatta na Moi aliyepokea hatamu za uongozi wa nchi, baada ya Kenyatta.
Mwai Kibaki alizaliwa mwaka 1931 na alikuwa serikalini kwa miongo mingi kama waziri, mbunge na hatimaye rais wa Kenya. Ameacha watoto wanne na wajukuu kadhaa.