1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Ujerumani asema taifa linakabiliwa na nyakati ngumu

28 Oktoba 2022

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameonya juu ya miaka migumu inayoikabili nchi hiyo na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua kuhusu mabadiliko ya tabianchi huku akiahidi kuendelea kutoa msaada kwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4IoBM
Deutschland | Bundespräsident Steinmeier | Rede an die Nation
Picha: Michele Tantussi/REUTERS

Hotuba hiyo ya Steinameier,ambayo ilikuwa na kaulimbiu isemayo; kinachotuunganisha kinatufanya kuwa imara zaidi, imekuja wakati Ujerumani ikiwa njiapanda, na rais huyo amegusia masuala kadhaa yalio vichwani mwa watu wengi nchini humo. Masuala hayo ni pamoja na mzozo wa gharama za maisha katikati mwa mfumuko wa bei unaozidi, mzozo wa nishati pamoja na vita vinavyoendelea nchini Ukraine.

"Jambo moja liko wazi: Tutalaazimika kukubali kujinyima kwa sehemu fulani kifedha katika miaka michache ijayo. Watu wengi wamekuwa wakihisi hili kwa muda mrefu. Kila mmoja laazima achangie pale wanapoweza. Mzozo huu unatuhitaji kujifunza kuishi maisha ya kawaida tena."

Rais Steinmeier amesema viwango vya umaskini vinaanza kupanda tena nchini Ujerumani, na kusisitiza hata hivyo kwamba hii siyo kebehi kwa maskini, lakini kuwaomba wale wanaoweza kujitolea kufanya hivyo. Ameuhakikishia umma kwamba serikali itasaidia wale wenye uhitaji zaidi kwa kadiri innavyowezekana.

Ukraine Kiew | Bundespräsident Steinmeier und Wolodymyr Selenskyj
Frank-Walter Steinmeier na rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskiyPicha: GLEB GARANICH/REUTERS

Akizungumzia ukosoaji wa hivi karibuni kwamba Ujerumani inafanya maamuzi yanayoiweka juu ya washirika wake wa Umoja wa Ulaya, kama vile mpango wa uokozi wa nishati, rais huyo amewahakikishia washirika kwamba Ujerumani inakubali wajibu wake katika jumuiya ya NATO na barani Ulaya, na kuongeza kuwa hii imedhihirishwa na  maamuzi ya sera ya usalama yaliochukuliw ana serikali ya Ujerumani tangu mabadiliko ya kihistoria Februari 24. Steinmeier pia amegusia changamoto za baadae kwa Ujerumani, hasa mabadiliko ya tabianchi.Rais Steinmeier aungwa mkono na chama kikuu cha upinzani

"Bila mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, yote haya hayatakuwa na maana. Mapambano haya yanahitaji nguvu zetu sote. Tudhihirishe nguvu yetu kwa kubadilika sasa! Tuwawezeshe watoto wetu kuishi vizuri kwenye sayari yetu. Hii iko mikononi mwetu!

Changamoto nyingine ya sasa na ya baadae alioigusia Steinmeier, ni kuhusu ulinzi wa demokrasia, dhidi ya mashambulizi ya ndani na nje. Amesema demokrasia haiwezi kufanya kazi bila mshikamano, na mshikamano laazima uje kwa vitendo. Hotuba ya Steinmeier imehudhuriwa na wawakilishi kutoka mashirika mbalimbali serikali, pamoja na yale yasiyo ya kiserikali na watu wenye umri mdogo kutoka kote Ujerumani.

Deutschland | Internationale Expertenkonferenz zum Wiederaufbau der Ukraine
Picha: Michele Tantussi/REUTERS

Hata hivyo Kansela Olaf Scholz, ambaye pia ni mwanachama cha chama cha Steinmeier, cha Social Democratic, SPD hakuhudhuria tukio hilo, na hakuna hata mmoja kati ya mawaziri wa Scholz amehudhuria, wala spika wa bunge Bärbel Bas, pia kutoka chama cha SPD.Marais wa Ujerumani na Ukraine wasuluhisha mzozo wao

Hotuba ya Steinmeier imekuja muda mfupi baada ya ziara yake ya kwanza mjini Kyiv, tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwezi Februari. Mwanzoni mwa vita hiyo, rais Steinmeier alikosolewa kwa msimamo wake uliochukuliwa kuwa laini kuhusu Urusi, ikiwemo kuituhumu NATO kwa kueneza uvumi wa vita dhidi ya Urusi mnamo mwaka 2016 na kuunga mkono mradi wa bomba la gesi la Nord Stream 2.

Rais ameomba radhi tangu wakati huo na kuelezea majuto kuhusu misimamo hiyo, na kusema rais wa Urusi Vladmir Putin anapaswa kushtakiwa kwa uhalifu wa kivita.