Rais wa Nigeria atangaza punguzo la bei ya mafuta ya petroli
16 Januari 2012Rais Jonathan ametangaza hatua hiyo katika hotuba yake kwa taifa kwa njia ya televisheni baada ya wiki ambayo amekuwa kimya , wakati mgomo na maandamano ya umma yakizuwia shughuli muhimu katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya wakaazi katika bara la Afrika , ambayo ni mtoaji mkubwa wa mafuta katika bara hilo.
Rais amedai kuwa maandamano yametekwa nyara na watu ambao amewaeleza kuwa wanataka kuchochea hali ya kutokuelewana , unaharibifu na hali ya kutokuwa na usalama . Rais Jonathan hakutoa maelezo zaidi katika madai yake hayo , lakini hotuba yake inaonyesha ni jinsi gani serikali yake imekuwa na wasi wasi kutokana na maandamano yanayoikumba nchi hiyo.
Rais Goodluck Jonathan katika hotuba yake leo asubuhi amesema kuwa serikali itatoa ruzuku kwa bei ya petroli ili kupunguza haraka bei ya mafuta hadi kiasi cha dola 2.75 kwa galoni huku kukiwa na mgomo wa nchi nzima ambao umeathiri taifa hilo la Afrika magharibi.
Serikali itaendelea na hatua yake ya kuibinafsisha sekta ya mafuta. Hata hivyo kutokana na matatizo yaliyowakabili Wanigeria , na baada ya kutafakari na kujadiliana na magavana wa majimbo na uongozi wa bunge , serikali imeidhinisha upunguzaji wa bei ya mafuta hadi naira 97 kwa lita.
Hotuba ya Jonathan inakuja baada ya jaribio lake la kufanya majadiliano na vyama vya wafanyakazi kushindwa jana jumapili kumaliza mgomo ambao unaingia siku yake ya sita leo. Rais wa chama kikuu cha wafanyakazi nchini Nigeria Abdulwaheed Omar amesema mapema leo Jumatatu kuwa amesitisha kwa muda maandamano yaliyopangwa kufanyika leo Jumatatu baada ya rais Jonathan kutangaza punguzo hilo la bei ya mafuta .
Mgomo ulianza Januari 9 na kusababisha shughuli kusita katika taifa hilo lenye wakaazi wanaofikia milioni 160.
Mzizi wa fitina unabaki kuwa bei ya mafuta. Serikali ya Goodluck Jonathan iliondoa ruzuku katika bei ya mafuta , ruzuku ambayo inaweka bei ya mafuta kuwa chini.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / ape
Mhariri : Mohammed Khelef