Rais wa Iran kuizuru Pakistan kusawazisha mivutano
21 Aprili 2024Taarifa ya wizara ya mambo ya kigeni ya Iran imesema Raisi ataandamana na ujumbe wa ngazi ya juu unaojumuisha waziri wa mambo ya nje, pamoja na ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara.
Mashambulizi ya kulipiza kisasi mwezi Januari katika eneo la mpakani la Balochistan lililogawanyika kati ya mataifa hayo mawili, yaliongeza mivutano ya kikanda iliyokuwa tayari imechochewa na vita vya Israel na Hamas. Tehran ilifanya mashambulizi dhidi ya kundi linaloipinga Iran nchini Pakistan katika wiki ambayo iliiyashambulia maeneo ya Iraq na Syria.
Pakistan ilijibu kwa kuyavamia maeneo ya kijeshi katika mkoa wa Iran wa Sistan-Balochistan, mojawapo ya maeneo machache yenye Waislamu wa Kisunni katika nchi ya Iran iliyo na Washia wengi. Iran na Pakistan katika siku za nyuma zimetuhumiana kwa kuwahifadhi wanamgambo.
Raisi pia atazuru Lahore na Karachi kukutana na wakuu wa mikoa hiyo. Nchi hizo mbili zitaimairisha uhusiano na kuboresha ushirikiano wa kibiashara, nishati, kilimo. Pakistan pia inategemea mradi wa pamoja wa gesi na Iran kutatua mzozo wa muda mrefu wa umeme ambao umeathiri ukuaji wa uchumi wake.