1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroPakistan

Kwa nini Pakistan na Iran ziliingia katika mzozo?

20 Januari 2024

Pakistan na Iran zimefanya mashambulizi ya kuvuka mpaka kwa kile wanachodai ni kukabiliana na makundi ya wanamgambo na hivyo mahusiano kati ya majirani hao kuingia katika hali ya mvutano.

https://p.dw.com/p/4bUzr
Pakistan, Islamabad | Mumtaz Zahra Baloch
Msmeaji wa wizara ya mambo ya nje ya Pakistan Mumtaz Zahra Baloch akizungumzia mzozo kati ya Pakistan na Iran Januari 18, 2024. Majirani hao wamesuluhisha tofauti zao.Picha: Muhammet Nazim Tasci/Anadolu/picture alliance

Tukianza na wale walioshambuliwa na Pakistan nchini Iran, waliolengwa ni wanaharakati wanaotaka kujitenga wanaofahamika kama Baloch katika Jimbo la Sistan-Baluchestan ambalo linapakana na Pakistan. Jeshi la Pakistan limesema magaidi hao ni kutoka kundi linalojiita "Jeshi la Ukombozi wa Baluchistan" yaani "The Baloch Liberation Front" (BLF).

Wanamgambo hao wa kabila la Baloch wanapambania uhuru wa jimbo la magharibi la Pakistan la Balochistan na wamekuwa wakipigana na serikali ya Islamabad kwa miongo kadhaa huku wakiituhumu serikali mjini Islamabad kuwa inanyonya rasilimali nyingi za gesi na madini katika jimbo hilo linalopakana na Afghanistan na Iran.

Soma pia:Waziri Mkuu wa Pakistan kuongoza mkutano wa usalama kuangazia mashambulizi kati yao na Iran

Wanamgambo wa BLF ni miongoni mwa waasi ambao mara kadhaa huilenga miradi ya gesi miradi na vituo vya maafisa wa usalama lakini hivi karibuni wameanza pia mashambulizi katika maeneo mengine ya Pakistan. Pia huishambulia miradi mbalimbali inayosimamiwa na China na mara kwa mara wamekuwa wakiwaua wafanyakazi raia wa China licha ya Pakistan kuhakikisha kwamba inafanya kila iliwezalo ili kulinda miradi hiyo ya China.

Balochistan ina umuhimu gani?

Mzozo mpya kati ya Pakistan na Iran
Mkaazi wa eneo la Balochistan akionyesha mlima uliopo Koh-e-Sabz katika eneo la Pakistan :17.01.2024Picha: Banaras Khan/AFP/Getty Images

Balochistan ni mkoa mkubwa wa milimani wenye jangwa na wenye takriban watu milioni 15.  Jimbo hilo lina utajiri mkubwa wa madini ambayo kwa kiasi kikubwa bado haujashughulikiwa. Ni jimbo kubwa zaidi nchini Pakistan lakini lenye idadi ndogo kabisa ya watu kulingana na majimbo mengine. Eneo hilo Iinapakana na mkoa wa Sistan-Baluchestan wa Iran ulioshambuliwa na Pakistan.

Katika wiki za hivi karibuni, Mamia ya waandamanaji wa kabila la Baloch, wengi wao wakiwa wanawake waliandamana katika mji mkuu wa Pakistan wa Islamabad huku wakiishutumu serikali kwa kuwakandamiza watu katika jimbo hilo, kwa kuendesha vitendo vya kinyama ikiwa ni pamoja na utekaji nyara na mauaji.

Balochistan ni eneo muhimu kwa mradi wa mabilioni ya dola unaofahamika kama Ukanda wa Kiuchumi wa China na Pakistani (CPEC). China imetekeleza miradi ya uchimbaji madini na kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa katika mji wa pwani wa kusini mwa jimbo hilo wa Gwadar.

Soma pia:Pakistan imeihimiza Iran kuimarisha ushirikiano baada ya mashambulizi ya makombora

Kampuni ya uchimbaji madini ya Canada ya "Barrick Gold" inamiliki asilimia 50 ya hisa katika katika Mgodi wa Reko Diq wilayani Chagai katika mkoa huo, huku hisa zilizobaki zikimilikiwa na serikali ya Pakistan na mamlaka ya mkoa. Kampuni ya Barrick inauchukulia mgodi huo kuwa miongoni mwa migodi mikubwa zaidi duniani ambayo bado haijachimbwa na iliyo na utajiri mkubwa wa madini ya shaba na dhahabu.

Kundi lililopo Pakistan lililolengwa na mashambulizi ya Iran

Iran ilisema Jumanne wiki hii kuwa iliendesha mashambulizi ya makombora na droni nchini Pakistan na kulilenga kundi la wanamgambo ambalo ilidai kuwa na mafungamano na Israel.

Waziri Mkuu wa muda wa Pakistan akiongoza mkutano wa dharura mjini Islamabad
Waziri Mkuu wa muda wa Pakistan akiongoza mkutano wa dharura mjini Islamabad:19.01.2024Picha: PID/Handout via Xinhua/picture alliance

Kundi hilo ni Jaish al-Adl (JaA) ambao ni mwanamgambo wenye msimamo mkali  wa Kiislamu wa dhehebu la Sunni. Kundi hilo lilitokana na lile la Jundallah, lililoanzishwa na kuongozwa na Abdolmalek Rigi mnamo mwaka 2002 kabla ya kuuawa na Serikali ya Iran mwaka 2010.

Baada ya kifo cha Rigi, vikundi kadhaa viliundwa huku JaA likiibuka kuwa lenye ushawishi mkubwa. Kundi hilo linaendesha shughuli zake kusini mashariki mwa Iran na magharibi Jimbo la Pakistan la Balochistan linalopakana na mataifa ya Iran na Afghanistan kulikoripotiwa mashambulizi ya wiki hii.

Chanzo: (RTRE)