1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran na Kenya kuimarisha uhusiano wa nchi zao

12 Julai 2023

Rais wa Iran Ebrahim Raisi amepokea makaribisho ya hali ya juu kutoka kwa mwenzake wa Kenya William Ruto siku ya Jumatano katika ziara ya nchi tatu za Afrika.

https://p.dw.com/p/4TlR5
Iranischer Präsident Ebrahim Raisi in Kenia
Rais wa Iran Ebrahim Raisi akikagua guaride la heshima katika Ikulu ya NairobiPicha: Khalil Senosi/AP/picture alliance

Viongozi wa Iran na Kenya wamesisitiza juu ya kuimarisha uhusiano wa nchi zao wakati walipotia saini makubaliano ya kibiashara leo hii Jumatano. Rais wa Iran Ebrahim Raisi anafanya ziara yake ya kwanza katika taifa hilo la Afrika Mashariki na ameelezea ziara yake nchini Kenya kuwa ni kipindi cha mabadiliko na maendeleo katika uhusiano baina ya nchi hizo mbili. Amesema mazungumzo yake na Rais wa Kenya William Ruto yameonesha azma kamili ya nchi zote mbili ya kuongeza ushirikiano wa kiuchumi, kibiashara, kisiasa na utamaduni.

Rais wa Kenya William Ruto.
Rais wa Kenya William Ruto.Picha: DW

Kwa upande wake, Ruto ameielezea Iran kuwa ni mshirika muhimu wa kimkakati kwa Kenya na amesema serikali hizo mbili zimetia saini mikataba mitano ya maelewano inayolenga sekta mbalimbali ikiwemo ya teknolojia ya habari, kukuza uwekezaji na uvuvi. Rais wa Kenya amesema makubaliano hayo yataimarisha uhusiano na yatakuwa chachu ya maendeleo endelevu kati ya nchi hizo mbili.

Ziara hiyo ya kiongozi wa Iran inaambatana na juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kutafuta uungwaji mkono katika kuondoa mkwamo wa kidiplomasia ambapo nchi hiyo imetengwa kimataifa.

Rais wa Iran Ebrahim Raisi
Rais wa Iran Ebrahim RaisiPicha: Iranian Presidency Office/APAimages/IMAGO

Rais Ibrahim Raisi pia anatarajiwa kwenda Uganda na Zimbabwe wiki hii katika ziara ya kwanza barani Afrika kuwahi kufanywa na kiongozi wa Iran katika kipindi cha miaka 11. Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran, IRNA, Rais Ibrahim Raisi ameandamana na ujumbe unaowajumuisha waziri wa mambo ya nje na wafanyabiashara wakuu.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Nasser Kanani hapo awali alielezea matumaini yake kuwa safari hiyo ya siku tatu barani Afrika inaweza kusaidia kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na mataifa ya Afrika.

Bara la Afrika limekuwa uwanja wa mapambano ya kidiplomasia katika miezi ya hivi karibuni, wakati ambapo Urusi na nchi za Magharibi zikijaribu kutafuta kuungwa mkono na nchi za Afrika kuhusu vita vya Ukraine, ambavyo vimekuwa na athari mbaya za kiuchumi katika bara hilo. Athari hizo zimesababisha bei za vyakula kupanda.

Mataifa yenye nguvu ya Magharibi pia yamezidisha uhusiano wa kibiashara na bara la Afrika sawa na India na China, ambayo imewekeza pakubwa katika miundombinu barani Afrika.

Vyanzo: RTRE/AFP/AP/DPA