1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa China Xi Jinping aanza ziara ya siku tatu Urusi

20 Machi 2023

Rais wa China Xi Jinping amewasili Moscow kuonesha mshikamano wa kidiplomasia na kisiasa kwa mwenzake wa Urusi Vladimir Putin dhidi ya nchi za Magharibi, siku chache baada ya waranti wa kukamatwa Putin kutolewa na ICC.

https://p.dw.com/p/4Oww5
Russland Präsident Xi und Putin
Picha: Sergei Karpukhin/Sputnik/REUTERS

Mataifa hayo mawili China na Urusi yaliyo na nguvu duniani, yameielezea ziara ya Xi ya siku Tatu kama nafasi ya kuimarisha urafiki wao usiokuwa na mipaka. China inaitegemea  Urusi kama chanzo chake cha  mafuta na gesi kwaajili ya kuuendeleza uchumi wake unaotegemea pakubwa nishati hizo muhimu. China pia inaiona Urusi kama mshirika katika kukipinga  kile ambacho wote wanaamini ni kujiingiza kwa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi tofauti duniani.

China yahimiza amani Ukraine baada ya Marekani kusema inaisaidia Urusi

Nchi hizo mbili ambazo ni miongoni mwa nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia zimewahi kushiriki luteka ya pamoja. Kulingana na msemaji wa ikuluya Urusi Dmitry Peskov viongozi hao wawili watajadili kwa upana operesheni ya Urusi nchini Ukraine huku mazungumzo mengine mapana na muhimu yakitarajiwa kufanywa hapo kesho Jumanne 21.03.2023.

Kwa Putin ujio wa Xi ni ushindi wa kidiplomasia unaotuma ujumbe kwa Viongozi wa mataifa ya Magharibi ambao ni washirika wa Ukraine kuwa juhudi zao za kumtenga zinaambulia patupu na kwamba mataifa hayo mawili hayako tayari kukubali hatua za kujaribu kuyadhoofisha.

Urusi yasema ICC haina haki yoyote yakisheria kuishurutisha

Niederlande Den Haag | Haager Tribunal | International Criminal Court | Prozess Mahamat Said Abdel Kani | Chefankläger Karim Khan
Mwendesha mashitaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC Karim KhanPicha: Peter Dejong/AP Photo/picture alliance

Ziara ya Xi inajiri wakati mwendesha mashitaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC iliyoko mjini The Hague Uholanzi Karim Khan kutangaza siku ya Ijumaa kwamba wamechukua hatua dhidi ya Putin kufuatia madai ya kuhusika na uhalifu wa kivita nchini Ukraine na kutoa waranti wa kukamatwa kwake.

Biden, ameupongeza uamuzi wa mahakama ya ICC

ICC ilidai Putin aliwaondoa maelfu ya watoto Ukraine, madai ambayo Moscow inayakanusha huku ikiitaka ICC kuheshimu kinga ya kutoshtakiwa kwa wakuu wake wa serikali. Urusi imedai kuwa ICC haina nguvu yoyote kisheria kuishurutisha kwa lolote maana sio mwanachama wa ICC.

EU yatoa silaha zaidi kwa Ukraine

Belgien | Treffen EU-Außenminister | Runder Tisch
Kikao cha Mawaziri wa nchi za nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels Picha: European Union

Huku hayo yakiarifiwa Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wamesema nchi 27 wanachama wa Umoja huo zimekubaliana kutoa risasi na makombora milioni moja kwa Ukraine kwa miezi 12 huku Kiev ikiendelea kuomba silaha zaidi ili kupambana na uvamizi wa Urusi.

Zelensky ashinikiza uharakishaji wa kuepeleka silaha Ukraine

Nchi hizo zitapeleka silaha hizo haraka iwezekanavyo kutoka kwenye  akiba zao. 

Katika mkutano huo uliofanyika mjini Brussels, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Catherine Colonna amesisitiza kwamba ni lazima umoja huo utoe usaidizi wa kutosha kwa Ukraine. Makubaliano hayo yamekuja wakati kukiwa na wasiwasi kwamba Ukraine inaweza kuishiwa na silaha katika siku za usoni kutokana na vita vinavyoendelea.

Chanzo: afp/ap/reuters