1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza aelekea Uganda kwa mazungumzo na rais Yoweri Museveni juu ya ujumbe wa kusimamia amani nchini Somalia.

28 Mei 2009

Wanajeshi 4,300 kutoka Burundi na Uganda ndio wanaoilinda serikali ya mpito nchini Somalia.

https://p.dw.com/p/HzcY
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.Picha: AP

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza alikua akitarajiwa kuwasili nchini Uganda leo kwa mazungumzo na mwenyeji wake juu ya kuendelea kwa ujumbe wa kusimamia amani nchini Somalia. Burundi na Uganda ndizo pekee zilizochangia wanajeshi hadi sasa katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia.

Rais Nkurunziza na mwenzake Yoweri Museveni wa Uganda watazungumzia juu ya azimio la hivi karibuni la umoja wa mataifa, kurefusha muda wa kuwepo jeshi la kusimamia amani la Umoja wa Afrika nchini Somalia -AMISOM- hadi Januari mwaka ujao 2010.

Kuna kiasi ya wanajeshi 4.300 wa Burundi na Uganda ambao wanailinda serikali ya mpito ya Somalia inayoongozwa na Rais Shariff Sheikh Ahmed na ambayo inazidi kukumbwa na hujuma kali za wapiganaji wa kiislamu wenye msimamo mkali.

Jeshi hilo la umoja wa Afrika lilikuwa liwe na wanajeshi 8.000, lakini mpaka sasa ni Burundi na Uganda pekee zilizochangia wanajeshi, huku mataifa mengine ya kiafrika yalioahidi yakishindwa kufanya hivyo.

Hali nchini Somalia tangu tarehe 7 ya mwezi huu wa Mei imezidi kuwa tete, kukizuka mapigano makali na makundi ya Kiislamu ya msimamo mkali Al-Shabaab na Hizbul Islam yakijaribu kusonga mbele kwa lengo la kuuangusha utawala wa Rais Sheikh Ahmed mwenye msimamo wa wastani.

Islamischer Kämpfer in Somalia
Mmoja wa wanamgambo nchini Somalia.Picha: AP

Zaidi ya watu 200 wengi wao wakiwa raia wameuwawa na karibu 7.000 kuyakimbia makaazi yao wakatafuta hifadhi kaskazini mwa mji mkuu Mogadishu.

Rais huyo mpya aliingia amadarakani mapema mwaka huu kama sehemu ya utaratibu wa kusaka amani uliosimamiwa na Umoja wa mataifa. pamoja na hayo serikali yake mpaka sasa inaidhibiti sehemu ndogo tu ya mji mkuu, wakati wapiganaji wa Kiislamu wanayadhibiti maeneo makubwa ya kusini na katikati mwa Somalia.

Kukutana kwa marais Nkurunziza na Museveni nchini Uganda hii leo kwa upande mwengine, kumekuja katika wakati ambao wapiganaji wa kiislamu wameonya juu ya uamuzi wa umoja wa mataifa kurefusha muda wa jeshi la kusimamia amani la umoja wa Afriaka nchini Somalia. Wapiganaji hao wamesema uamuzi huo uatazusha janga zaidi nchini humo, wakiapa kuendelea na mapigano.

rais Sharif Ahmed jana aliishutumu Eritrea akisema ndiyo yenye kuwapa sehemu kubwa ya silaha wapiganaji hao madai ambayo Eritrea imeyakanusha.

Umoja wa Afrika na jumuiya nyengine zimetoa wito wa vikwazo dhidi ya Eritrea na katibu mkuu wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Uganda James Mugume amesema suala hilo huenda pia likazungumzwa na marais wa Uganda na Burundi katika mkutano wao wa leo.

Hali hii mpya ilizuka baada ya majeshi ya Ethiopia yalioingia Somalia kuwaondoa wapiganaji wa muungano wa mahakama za kiislamu, kuihama Somalia mwishoni mwa mwaka jana.

Somalia imekua haina serikali madhubuti tangu ulipoangushwa utawala wa rais wa zamani Mohamed Siad Barre 1991 na kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Jason Nyakundi/DPAE

Mhariri:M.Abdul-Rahman