Rais Putin azuru Vietnam, nini kinatarajiwa huko?
19 Juni 2024Rais Putin anazuru mji mkuu wa Vietnam kwa mwaliko wa Katibu Mkuu Chama cha Kikomunisti nchini Vietnam Nguyen Phu Trong. Nchi hiyo inatarajia nini kutoka kwa Putin ambaye pamoja na mengineyo anakabiliwa na vizuizi na waranti wa kukamatwa wa mahakama ya ICC?
Kesho Alhamisi, Rais Vladimir Putin atakaribishwa rasmi katika hafla itakayofanyika kwenye Makazi ya Rais, kabla ya kushiriki mazungumzo kati yake na Mkuu wa Chama cha Kikomunisti Nguyen Phu Trong. Atakutana pia na Waziri Mkuu wa Vietnam Pham Minh Chinh pamoja na Wavietinam wanaosoma Urusi. Jioni, atahudhuria dhifa ya kitaifa.
Putin anajaribu kukabiliana na athari za kutengwa kwenye majukwaa ya kimataifa, kwa kusaka uungwaji mkono wa washirika wake waliosalia. Anakwenda Vietnam yenye mahusiano mazuri na Umoja wa Ulaya na Marekani, ambayo tayari imekosoa vikali ziara hiyo ya Putin mjini Hanoi.
Soma pia: Korea K., Urusi zasaini mkataba wa ushirikiano wa kimkakati
Ingawa haijulikani nini ambacho Hanoi inakitarajia, lakini wafuatiliaji wanapendekeza kwamba ziara hii fupi ya Putin huko Vietnam na Korea Kaskazini ni muhimu na inatoa ishara kubwa.
Putin alenga kuimarisha uhusiano na washirika waliosalia
Profesa wa masuala ya siasa Carl Thayer na mchambuzi wa masuala ya Vietnam wa chuo Kikuu cha New South Wales cha nchini Australia anasema Putin ananuia kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na mahusiano ya kiuchumi kupitia biashara na ahadi za uwekezaji kwa kutumia sarafu ya rubble.
Lakini mchambuzi mwingine kutoka Kituo cha Masomo ya Usalama cha Asia-Pasifiki kilichoko Hawaii Alexander Vuving anasema Urusi inataka kutuma ujumbe kwamba ina marafiki kila mahali ulimwenguni kwa hivyo juhudi za magharibi za kuitenga ni kama kelele za chura, ambazo hazimzuii ng'ombe kunywa maji.
Ameongeza kwamba Hanoi ina maslahi makubwa tu, zaidi ya mizizi ya Ukomunisti inayokutanisha nchi hizo mbili. Akasema Urusi ina jukumu kubwa si tu katika sera ya nje ya Vietnam lakini pia ni muuzaji mkubwa wa silaha nchini humo.
Vietnam linakuwa taifa la tatu kutembelewa na Putin baada ya China na Korea Kaskazini tangu aliporejea madarakani mnamo mwezi Mei. Amesafiri mara chache tangu Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC ilipotoa waranti wa kukamatwa kutokana na madai ya uhalifu katika vita vya nchini Ukraine. Hii ni mara ya kwanza kuzuru Vietnam tangu mwaka 2017 na mara ya tano kwa ujumla.
Urusi na Vietnam wana uhusiano wa kihistoria
Mataifa haya yana mahusiano ya kihistoria yanayoanzia kwenye misingi ya Ukomunisti. Maelfu ya makada wamesoma katika uliokuwa Umoja wa Kisovieti wakati wa Vita Baridi, miongoni mwao ni mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam Nguyen Phu Trong.
Soma Pia:Putin aipongeza Korea Kaskazini kwa msaada wake katika vita
Gazeti la serikali la Vietnam la Bao Moi limeandika kwenye moja ya makala zake kwamba Rais Putin ni mtu mwenye mchango mkubwa katika uhusiano wa mataifa hayo na wakati wote amekuwa akionyesha nia njema.
Lakini Hanoi, ambaye ni mshirika wa Marekani ana kila sababu ya kuwaweka hatarini washirika wake wa kidiplomasia kutokana na ziara hii, anasema Ian Storey, wa taasisi ya masuala ya kijamii, kisiasa na usalama ya ISEAS-Yusof Ishak iliyopo Singapore.
Anasema, Hanoi inataka Putin afike huko kwa sababu kadhaa, na kubwa ni kuonyesha kwamba Vietnam inatekeleza sera ya nje ya usawa na isiyoegemea taifa lolote lenye nguvu ama "Bamboo Diplomacy."
Ziara hii ya Putin inahitimisha ziara za viongozi wa kile kinachotizamwa kama mataifa matatu makubwa ama "Big Three". Rais Joe Biden alianza kuzuru taifa hilo akifuatiwa na Rais wa China Xi Jinping miezi michache baadae.
Kunatarajiwa kutangazwa makubaliano ya kijeshi, kibiashara, uwekezaji, teknolojia na elimu, hii ikiwa ni kulingana na maafisa waliozungumza na Reuters wiki hii.