Rais Ruto wa Kenya aanza kuteua baraza jipya la mawaziri
19 Julai 2024Ruto ametangaza orodha ya wanasiasa anaowapendekeza kushika nyadhifa za uwaziri kupitia hotuba yake kwa taifa aliyoitoa majira ya Alasiri. Tangazo hilo ni sehemu ya juhudi zake za hivi karibuni kabisa za kutuliza joto la mzozo mbaya zaidi ulioukumba utawala wake wa miaka miwili.
Katika hotuba yake kwa taifa, Rais Ruto ametangaza majina 11 ya wanasiasa anaowapendekeza kuwa mawaziri pamoja na jina moja la mtu anayependekeza kuchukua wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
"Ingawa matukio ya mwezi uliopita yalisababisha vurumai, wasiwasi na kukosekana mwelekeo, mzozo ule umetupatia nafasi kubwa, kama taifa, kuanzisha muungano wa pamoja unaojumuisha kada zote za taifa leo kwa ajili ya mageuzi na kusonga mbele," amesema Rais Ruto.
"Hatimaye, nimeanza safari ya kuunda upya Baraza la Mawaziri linalojumuisha pande zote ili lisaidie kuleta mabadiliko makubwa na ya haraka yanayohitajika nchini mwetu."
Baadhi ya mawaziri waliokuwa baraza lililovunjwa wajitokeza baraza jipya
Mawaziri aliowapendekeza ni lazima waidhinishwe na Bunge. Hata hivyo miongoni mwa wale waliopendekezwa walikuwa sehemu ya baraza alilolivunja karibu wiki mbili zilizopita ikiwemo Kithure Kindiki aliyokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, iliyokuwa ikisimamia Polisi ya Kenya ambayo imelaumiwa sana kwa kufanya ukandamizaji wakati wa maandamano.
Kindiki sasa ameteuliwa kuwa waziri wa masuala ya ndani, Aden Duale waziri wa ulinzi, Debra Mulongo Barasa - Afya, Alice Wahome - Ardhi, Davis Chirchir - Uchukuzi, Soipan Tuya - Mazingira, Julius Migosi - Elimu, Eric Muriithi - Maji, Margaret Ndungu - Teknolojia, Andrew Karanja - Kilimo na Rebecca Miano atahudumu kama Mwanasheria Mkuu.
Muungano wa upinzani wa Azimio umekwishasema hautajiunga na serikali yoyote ya umoja wa kitaifa ambayo Ruto atajaribu kuuiunda.
Taifa hilo la Afrika Mashariki limekumbwa na wimbi la maandamano ya umma ya mwezi mzima ambayo yalianza kama mikusanyiko ya amani dhidi ya Muswada wa Fedha 2024/2025.
Muswada huo uliokuwa unajumuisha pendekezo la kuanzisha mkururo wa kodi, ushuru na tozo ulipingwa na umma wa nchi hiyo kupitia wimbi kubwa la maandamano yaliyoongozwa na makundi ya vijana wa kizazi kipya maarufu Gen-Z.