Rais mteule wa Argentina azungumza na maafisa wa Marekani
29 Novemba 2023Alikuwa amepangiwa kukutana na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani Jake Sullivan na afisa mwingine mwandamizi wa Baraza la Usalama wa Taifa.
Milei amewaambia waandishi habari alipokuwa akitoka ikulu ya White House kwamba mkutano wake umekuwa "mzuri" na ulijikita juu ya masuala ya uchumi na hali ya kijamii nchini Argentina.
Mwanasiasa huyo wa mrengo mkali wa kulia anatarajiwa kuapishwa mnamo Disemba 10 kuiongoza Argentina baada ya kushinda uchaguzi chini ya ahadi za mageuzi makubwa ya uchumi ikiwemo kuachana na sarafu ya nchi hiyo na kuanza kutumia dola ya Marekani.
Vilevile ameahidi hatua kali za kubana matumizi kwa dhamira ya kurekebisha uchumi unaochechemea ambao unazongwa na mfumuko mkubwa bei, akiba ndogo ya fedha za kigeni na kuanguka kwa shughuli za uzalishaji.