Rais Magufuli aahidi kufanya kazi na wapinzani Tanzania
1 Novemba 2020Rais wa Tanzania John Magufuli ameahidi kufanya kazi na wapinzani wake baada ya ushindi wa kishindo katika uchaguzi ambao mpinzani wake mkuu aliuelezea kuwa wa udanganyifu mkubwa na Marekani ikasema ulikumbwa na dosari nyingi.
Kauli ya Magufuli inakuja kabla ya maandamano ambayo upinzani umeyaitisha Jumatatu kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
"Nitakuwa mtumishi wa Watanzania wote. Ningependa kuwashukuru wagombea wenzangu wa urais kwa kushiriki," Magufuli alisema katika hafla ya mji mkuu Dodoma ambako alipokea rasmi matokeo.
Soma zaidi: Tume ya Uchaguzi Tanzania: Magufuli ndiye mshindi wa urais
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi Ijumaa, Magufuli alipata asilimia 84 ya kura dhidi ya mpinzani wake mkuu Tundu Lissu aliyepata asilimia 13.
"Ninaahidhi kufanya kazi nanyi ili kuhakikisha tunatekeleza maendeleo ya kitaifa. Maendeleo hayaegemei vyama...siasa sio vita, siasa sio mgogoro, sisi sote ni Watanzania."
Rais huyo mteule mwenye umri wa miaka 61 anatarajiwa kuapishwa rasmi Alhamisi wiki ijayo kuongoza kwa muhula wa pili wa miaka mitano.
"Wakati wa uchaguzi kulikuwa na changamoto chache lakini kwa jumla uchaguzi ulikuwa salama na wa amani," alisema Magufuli. "Huu ni muhula wangu wa pili na wa mwisho madarakani."
Soma pia: CCM inaendelea kuongoza katika hesabu ya kura
Kauli hiyo ya Magufuli ya kutowania kipindi kingine madarakani inatajwa kuwa ya umuhimu mkubwa kwa kuwa chama chake CCM, kimeshinda karibu viti vyote vya ubunge, jambo ambalo linakipa nguvu chama hicho kubadili katiba na kumpa ridhaa ya kuwania tena, hatua ambayo imekwisha anza kuzungumzwa na baadhi ya maafisa.
Magufuli anapokea cheti hicho cha ushindi ikiwa ni siku moja tu baada ya vyama viwili vya upinzani kuyapinga matokeo ya uchaguzi huo kwa kudai kulikuwa na udanganyifu mkubwa
Jumamosi, chama cha Lissu CHADEMA na chama kingine cha upinzani ACT Wazalendo vimeitisha maandamano yasiyo na kikomo ya kudai uchaguzi kuandaliwa upya.
Soma pia: Lissu asema hatambui matokeo ya udanganyifu
Ubalozi wa Marekani mjini Dar es Salaam ulisema kura zilikumbwa na madai ya dosari, ikiwemo matumizi ya nguvu dhidi ya raia wasiokuwa na silaha, upigaji kura bandia kabla ya uchaguzi, kuzuiliwa kwa maafisa wa upinzani na vizuizi dhidi ya mawakala wa vyama vya siasa kufika katika vituo vya kupigia kura.
Mwandishi: Bruce Amani
Reuters