1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Tanzania: Rais Magufuli achukua uongozi wa mapema

Hawa Bihoga29 Oktoba 2020

Rais John Magufuli aendelea kupata idadi kubwa ya kura zilizokusanywa kutoka katika majimbo mbalimbali ikiwemo yale yaliolalamikiwa na vyama vya upinzani kutokuwepo kwa usawa.

https://p.dw.com/p/3kbeh
Tansania Wahlen | Präsident John Magufuli
Picha: Ericky Boniphace/AFP

Tume ya taifa ya uchaguzi nchini Tanzania imeendelea kutoa matokeo ya uchaguzi wa nafasi ya urais huku mgombea wa chama tawala CCM na Rais anaetetea awamu yake kwa muhula mwingine akiendelea kupata idadi kubwa ya kura zilizokusanywa kutoka katika majimbo mbalimbali ikiwemo yale yaliolalamikiwa na vyama vya upinzani kutokuwepo kwa usawa. 

Ndani ya ukumbi huu ambao haujafurika idadi kubwa ya watu kama wengi walivyotarajia kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo waangalizi wa uchaguzi kutoka nje ya Tanzania kutokuwa wengi kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2015 uliomuweka mamlakani rais John Magufuli, waangalizi wa ndani, mawakala wa vyama vya siasa pamoja na wanahabari wanashuhudia mchakato huu wa kutoa matokeo.

Tangu kuanza kwa zoezi hilo majira ya asubuhi hii leo,hadi tunapoandaa ripoti hii tayari idadi ya majimbo takriban 50 yaliowasilisha matokeo yake ambayo kwa kiwango kikubwa bado yanaonekana kumpatia idadi kubwa ya kura mgombea wa chama tawala ccm ambae anawania muhula wa pili na wa mwisho John Magufuli.

Ilitarajiwa kuwa kungekuwa na ushindani mkali kati ya John Magufuli na Tundu Lissu
Ilitarajiwa kuwa kungekuwa na ushindani mkali kati ya John Magufuli na Tundu Lissu

Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi NEC jaji mstaafu Semistoklesi Kaijage, ameendelea kusoma matokeo hayo kadri yanavyowasilishwa kutoka katika majimbo mbalimbali hadi yatakapotimia 264 kwa mujibu wa tume ya uchaguzi ya taifa hilo.

Katika maeneo ambayo yalitazamwa kama kambi za upinzani ikiwemo katika baadhi ya majimbo ya mkoa wa Mara, mgombea wa CCM anaonekana kuvuna idadi kubwa ya kura, ikiwemo katika upande wa Tanzania Zanzibar ispokuwa kwa baadhi ya majimbo yaliopo Pemba ambako katika chaguzi kadhaa siasa zake zimeonekana kuwa ni za misimamo mikali.

Katika matokeo hayo yanayoendelea kutolewa ambayo yanapingwa hadharani na mgombea wa chama kikuu cha upinzani Tundu Lisu kwa madai kuwa zoezi la uchaguzi liligubikwa na kutokutendewa haki na uwazi kwa mawakala wa vyama vya upinzani unaendelea kuzua mjadala mpana katika mitandao ya kijamii.

Tundu Lissu ayapinga matokeo

Baadhi ya waangalizi wa ndani ambao wanaendelea kushuhudia mchakato huo wa utangazwaji wa matokeo ya awali akiwemo Frorent Rwakyoma ambaye ni mwenyekiti wa shirika la kiraia TEHE, ameiambia Dw wamesema, wanachoshuhudia katika zoezi hilo ni kile ambacho tume kinapokea kutoka katika majimbo ya uchaguzi maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo upande wa Zanzibar.

Katika hatua nyingine kamanda wa jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es salaam Lazaro Mambosasa mapema leo, ametembelea katika kituo hicho kinachoitangaza matokeo ya awali ya urais pamoja na vituo vingine vinavyotangaza matokeo ya nafasi ya ubunge na kuwaonya watu ambao wanayatwaa majukumu ya tume na kutangaza matokeo kuacha mara moja kadhalika kuonya vikalii kundi la watu litakalodhamiria kuingia barabarani kwa ajili ya kufanya maandamano.

Hadi sasa katika mkoa wa Dar es salaam matokeo ya kura za ubunge bado wapiga kura wameendelea kusubiri ispokuwa katika jimbo la kigamboni ambalo limeendelea kuongozwa na chama tawala kupitia dokta Faustine Ndugulile, huku katika majimbo kama vile Kawe ambalo siasa zake zilionekana kuwa na mvutano mkali kati ya mgombea anaetetea kiti chake Halima Mdee wa chama cha upinzani Chadema dhidi ya askofu Josephat Gwajima ambae ni mgombea wa ccm aliejitosa katika kinyang'anyiro hicho kwa mara ya kwanza.