Rais wa Madagascar ajiuzulu ili kugombea muhula wa pili
12 Septemba 2023Hatua hiyo ya kujiuzulu kwa rais Rajoelina sio ya kushangaza huko Madagaska kwa sababu ni wajibu wa kikatiba ikiwa rais aliyeko madarakani atawania muhula wa pili ni lazima ajiuzulu kwanza. Andry Rajoelina, mwenye umri wa miaka 49, alituma barua yake ya kujiuzulu kwa Mahakama siku ya Jumamosi baada ya kuthibitishwa na Mahakama Kuu ya Kikatiba kama mgombea wa urais.
Jambo jipya katika hali hii ni kwamba shughuli zote za kitaifa na majukumu ya rais yataendeshwa na waziri Mkuu kwa pamoja na serikali yake. Kikatiba Spika wa Seneti ndiye anatakiwa kutwaa mamlaka ya urais wakati mkuu wa nchi anapojiuzulu. Kwa mujibu wa taarifa iliotolewa na mahakama ya katiba ni kwamba Spika wa Seneti, Herimanana Razafimahefa, amekataa kuchukuwa madaraka kwa sababu zake binafsi.
''Kuna uwezekano wa kutokea mgogoro''
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mahakama Kuu ya Madagaska ilichapisha orodha rasmi ya wagombea urais. Kati ya wagombea 28 katika kinyang'anyiro hicho, 13 waliidhinishwa kugombea, akiwemo Andry Rajoelina na marais wawili wa zamani, Marc Ravalomanana na Hery Rajaonarimampianina. Upinzani umelalamikia mchakato wa maandalizi ya uchaguzi huo. Masy Goulamaly, mbunge na mgombea wa zamani wa urais amesema amejiondoa kwenye kinyanganyiro cha uchaguzi wa Novemba 9.
"Kuna hitilafu nyingi katika uchaguzi huu, ugombea wa rais wa sasa unathibitisha hili kwa kushindwa kuheshimu sheria, nadhani ndiyo maana kuna uwezekano wa kutokea mgogoro, hivyo napendelea kujitoa kwenye kinyanganyiro tuone nini kitafuata.", alisema Goulamaly.
Kasha ya uraia pacha
Rajoelina alichukua madaraka mwaka wa 2009 kufuatia mapinduzi ya kijeshi, yaliyomuondoa madarakani rais wa zamani Marc Ravalomanana. Mwaka 2013, Andry Rajoelina, alipigiwa marufuku kugombea lakini hatimaye alichaguliwa kuwa rais miaka mitano baadae, mnamo 2018.
Katika miezi ya hivi karibuni, rais Andry Rajoelina amekumbwa na kashfa juu ya uraia wake pacha wa Ufaransa na Madagaska. Taarifa hiyo ilifichuliwa mwishoni mwa Juni na vyombo vya habari.
Duru zinaelezea kuwa rais Rajoelina alichukuwa uraia wa Ufaransa mnamo 2014. Kwa mujibu wa katiba ya Madagascar, rais anadaiwa kupoteza uraia wake, na bila uraia huu, hawezi kuongoza nchi wala kuwa mgombea wa uchaguzi. Kashfa hiyo ya uraia pacha imepingwa vikali na chama cha chake cha kisiasa.
Siku ya Jumamosi Mahakama ya Kikatiba ilitupilia mbali rufaa iliyowasilishwa na vyama vitatu vya upinzani kutaka jina la Rajoelina litupiliwe mbali kwenye daftari ya wagombea kufuatia tuhuma hizo.