1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu milioni moja wakabiliwa na njaa Madagascar

21 Mei 2021

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International limetoa wito wa kuingiliwa kati suala la njaa nchini Madagascar na kutaka msaada wa haraka wa kibindamu upelekwe nchini humo.

https://p.dw.com/p/3tli2
Madagaskar I Armut und Hungersnot
Picha: Rijasolo/AFP/Getty Images

Mamilioni ya watu nchini humo wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na ukame. Madagascar inakabiliwa na ukame mbaya kabisa ambao haujawahi kuonekana katika kipindi cha miaka 40.

Zaidi wa watu milioni 1 wanakabiliwa na njaa kutokana na ukosefu wa chakula unaoshuhudiwa hivi sasa kusini mwa Madagascar,na shirika la Amnesty International limewatolea mwito wahisani,seriikali za kigeni na viongozi wa kikanda kutwaa jukumu la kutia msukumo wa juhudi za kupatikana msaada kuepusha janga la kibinadamu katika nchi hiyo.

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa,lile la chakula na kilimo FAO na lile la mpango wa chakula duniani WFP,wiki iliyopita yalitowa tahadhari ya dharura kwa jumuiya ya kimataifa juu ya mgogoro wa kibinadamu unaojitokeza huko Kusini mwa Madagascar.

Madagaskar I Armut und Hungersnot
Wananchi wa MadagascarPicha: Rijasolo/AFP/Getty Images

Tamara Léger, Mshauri wa shirika la kutetea haki za binadamu la kimataifa Amnesty International huko Madagascar amesema haki za watu zaidi ya milioni moja zinakabiliwa na kitisho hivi sasa kusini mwa nchi hiyo ambapo maelfu yao wako hatarini kufa kwa njaa na zaidi ya milioni moja wanakabiliwa na hali ngumu ya kupata chakula cha kutosha.

Hali inatisha na kunahitajika hatua za haraka za ushirikiano wa kikanda na kimataifa kusaidia kuepusha kile ambacho kinaweza haraka kugeuka kuwa janga kubwa la kibinadamu.

Mshauri huyo wa Amnesty International amesema viongozi wa kikanda na jumuiya ya kimataifa hawawezi kudiriki kukaa kimya na kutazama wakati watu wanakufa kwa njaa nchini Madagascar. Jumuiya ya kimataifa inapaswa kushirikiana na kukusanya msaada kuisadia nchi hiyo wakati huu inapohitaji msaada.

Hali ya ukosefu wa chakula ilianza kuwa mbaya mnamo mwezi Septemba mwanzoni mwa msimu wa kulima. Na mgogoro unajitokeza baada ya kanda hiyo kuandamwa na ukame kwa miaka mitatu mfululizo hali ambayo imeifanya Madagascar kushuhudia ukame mbaya zaidi ambao haujawahi kuonekana kwa kipindi cha miaka 40.

Madagaskar I  Hunger
Wakaazi wa manispaa ya Ifotaka, moja ya maeneo yanayokabiliwa na njaaPicha: RijasoloAFP/Getty Images

Kwa mujibu wa shirika la mpango wa chakula,WFP kiasi watu milioni 1.14 kusini mwa nchi hiyo wanakabiliwa na ukosefu mkubwa sana wa chakula na watu 14,000 kati yao wako katika hali ya kiwango cha kutisha cha janga kubwa la ukosefu wa chakula.

Wanawake na watoto ndio walioathirika zaidi kutokana na ukame na familia nyingi zimelazimika kuchukua hatua za kupindukia mipaka kuendelea kuishi kwa mfano kuuza mali zao na hata kuwatumikisha watoto. Inaelezwa kwamba watoto pia wanashindwa kwenda shule kutokana na njaa.

Vifo kadhaa vimeripotiwa kutokea katika baadhi ya vijiji lakini hakuna idadi inayojulikana ya vifo vilivyotokana na njaa.

Watu wanaoendelea kuishi huku wakivumilia njaa wamelieleza shirika la mpango wa chakula kuhusu namna wanavyojaribu kufanya kila wawezalo kuepuka kifo,ikiwemo kuepuka kula chakula cha kawaida na badala yake wanakula miti ya mshubiri na udongo. Hali ni mbaya zaidi hasa kwa watoto ambao wanakosa virutubisho vinavyohitajika na hivyo kuzuia ukuaji mzuri wa watoto hao.

(Vyanzo: Amnesty International)

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW